August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Yericko Nyerere ambana mbavu Mwigulu

Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi

Spread the love

MWIGULU Lameck Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi amepata wakati mgumu kujibu hoja zilizotolewa na Yericko Nyerere kuhusiana na hali ya usalama hapa nchini ikiwemo kupatikana kwa maiti za watu saba katika eneo la mto Ruvu mkoani Pwani, anaandika Wolfram Mwalongo.

Yericko ambaye ni mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi alikutana uso kwa uso na waziri Mwigulu katika kipindi cha ‘Tuongee asubuhi’ kinachorushwa na kituo cha Runinga cha Star TV.

Katika mahojiano hayo, Yericko amelilaumu Jeshi la Polisi nchini kwa madai kuwa limekuwa likijihusisha na propaganda za kisiasa tofauti na mataifa mengine hususan yaliyoendelea ambayo vyombo vyao vya ulinzi na usalama hujitenga na ‘chokochoko’ za kisiasa.

Akizungumzia sakata la kuokotwa kwa maiti katika eneo la Mto Ruvu mkoani Pwani, amesema ameshangazwa na jinsi mamlaka za serikali zilivyoshindwa kuchukua hatua madhubuti katika suala hilo.

“Serikali inasema maiti zilizopatikana Mto Ruvu zilikuwa za wahamiaji haramu, sasa mbona zilikuwa na majeraha na pia zilitoswa mtoni na baadaye zikazikwa kiholela? Je nchi ambazo watu hao wametokea zikihitaji taarifa za kina juu ya maiti hizo serikali ya Tanzania itasemaje?” amehoji Yericko.

Akijibu hoja hizo, waziri Mwigulu amesema, “Yericko asichukue tu kila habari ya juu juu anayoitoa katika vyanzo visivyoeleweka na kuanza kuziamini kwani suala la ulinzi na usalama ni nyeti. Njia wanazotumia wahamiaji haramu ni za hatari, vyombo vya usafiri wanavyotumia ni hatarishi na majeraha hayo wanayapata humo.”

Majibu ya waziri Mwigulu yamezua sintofahamu zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa taarifa zilizoripotiwa hivi karibuni zinasema polisi mkoani Pwani waliziokota maiti za watu sita na mwingine mmoja na kuzizika pasipo kuacha kielelezo chochote ikiwemo nguo au vipimo vya vinasaba (DNA).

Kitendo hicho cha Polisi kimelalamikiwa na baadhi ya watu waliopoteza ndugu jamaa na marafiki zao katika siku za hivi karibuni kwani walihitaji kuhakiki maiti hizo iwapo si za ndugu zao.

error: Content is protected !!