January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Yanga yatinga robo fainali Kagame

Mshambuliaji wa Yanga, Malimi Busungu akipiga kichwa mbele ya mabeki wa KMKM

Spread the love

PRESHA imeshuka. Klabu ya Yanga imefanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMKM ya Zanzibar, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa Kundi A, mabao yote ya Yanga SC yalipatikana kipindi cha pili, yakifungwa na Malimi Busungu na lile la kujifunga la beki wa KMKM,Khamis Ali.

Busungu alifunga bao lake la tatu katika mashindani hayo dakika ya 55 akimalizia pasi ya Mzimbabwe, Donald Ngoma aliyeitoa huku amebanwa na mabeki wa KMKM waliomuwekea ulinzi mkali leo. Khamis Ali alijifunga bao dakika ya 72 akiwa katika harakati za kuokoa mpira wa krosi uliopigwa na Ngoma huku akizongwa na Amissi Tambwe kwa nyuma.

Kwa matokeo hayo Yanga imefanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainali wakiwa wanashika nafasi ya tatu nyuma ya Knartoum N ya Sudan wanaoongoza kwa pointi zao saba sawa na Gor Mahia ya Kenya.

Katika mchezo wa mapema uliowakutanisha Gor Mahia na Khartum N ziligawana pointi baada ya sare ya 1-1.
Mechi za mwisho za Kundi A zitachezwa Jumapili, Yanga ikimaliza na Khartoum N na Gor Mahia ikicheza na Telecom. KMKM imemaliza mechi zake na pointi tatu zilizotokana na ushindi wa 1-0 dhidi ya vibonde Telecom ya Djibouti.

error: Content is protected !!