May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Yanga yapigwa tatu na Simba, yashushwa kileleni

Spread the love

 

TIMU ya Simba Queen imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, dhidi ya Yanga Princess kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Mchezo huo uliopigwa leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam huku ikishudia Yanga Princess wakipoteza mchezo wao wa kwanza kwenye Ligi hiyo.

Kwenye mchezo huo Simba iliandika bao la kwanza kupitia kwa Mwanahamisi Omary kwenye dakika ya 30, baada ya kupiga shuti la mbali lililomshinda mlinda mlango wa Yanga Princess.

Dakika 13 baadaye Opa Clement alifanikiwa kuiandikia Simba bao la pili kwa njia ya mkwaju wa penalti baada ya nahodha wa Yanga kushika mpira na kuoneshwa kadi nyekundu na kufanya mchezo huo kwenda mapumziko Simba wakiwa mbele kwa mabao mawili.

Kipindi cha pili kilirejea na Simba kufanikiwa kuandika bao la tatu kupitia kwa Joel Bukuru dakika ya 50 na bao hilo lilidumu mpaka mwisho wa mchezo.

Kwa matokeo hayo Simba inapanda kileleni kwenye msimamo wa Ligi hiyo kwa kuwashusha Yanga baada ya kukusanya pointi 39 wakicheza michezo 15, na nafasi ya pili ikishikwa na Yanga wenye pointi 38.

error: Content is protected !!