October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Yanga yamjia juu Morisson, wampiga faini

Bernard Morrison

Spread the love

UONGOZI wa klabu ya Yanga umempiga faini ya Sh. 1.5 Milioni nyota wake raia wa Ghana, Benard Morrison kwa kufanya mahojiano na mwandishi wa habari bila kutoa taarifa kwa klabu na kuzua hali ya sintofahamu juu ya mkataba wake. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea). 

Katika mahojiano hayo aliofanya na televisheni ya mtandaoni ya Global, Morrison ameeleza kuwa mkataba wake na klabu hiyo utamalizika mwezi wa saba huku akiwa bado hajaongeza mkataba mwengine.

Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Yanga imeeleza kuwa mchezaji huyo aliingia mkataba wa kwanza na timu hiyo tarehe 15 Januari, 2020,  kwa muda wa miezi sita huku kukiwa na kipengele cha kuongeza kama wataridhishwa na kiwango chako.

Klabu imeendelea kwa kueleza kuwa walimuongezea mchezaji huyo mkataba wa mara pili terehe 20 Machi, 2020 ukiwa mkataba wa miaka miwili ambao utafikia kikomo terehe 14 Julai, 2022. Mbele ya mwana sheria wa klabu ya Yanga pamoja na mwakilishi kutoka GSM, mhandisi Hersi Said.

Akiongea na kituo cha radio cha Wasafi FM, mwakilishi kutoka GSM Hersi Said, alisema kuwa mchezaji huyo alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga hadi 2022 baada ya ule wa awali kwisha mwezi ujao.

“Mchezaji alisaini mbele ya mwanasheria wa Yanga na mkabata huo umesajiliwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na pia Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) hilo halina mjadala,” alisema Hersi.

Aidha Hersi aliongezea kuwa mchezaji huyo alimfuata binafsi na kumwambia kuwa anataka kuvunja mkataba na Yanga kwa kuwa kuna timu zina mhitaji na zimempa ofa nzuri.

“Mchezaji baada ya kusaini mkataba huo ameonesha kupata ofa kubwa kutoka maeneo mengine na ofa hizo anazozipata zinaonekana ni kubwa kuliko ya klabu ya Yanga na hivyo alinifuata kutaka kuvunja mkataba,” aliongezea Hersi.

Klabu ya Yanga imeeleza kusikitishwa na mchezaji huyo kufanya mahojiano bila ruhusa ya uongozi akiwa kambini na kuongezea kuwa kama kuna timu inahitaji huduma yake wafuate taratibu za kisheria.

Yanga leo itashuka dimbani kuikabili Namungo FC, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara majira ya Saa 1 usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

error: Content is protected !!