January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Yanga yakwama tena safari ya Mauritius

Spread the love

SAFARI ya klabu ya Yanga kwenda Mauritius kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Cercle de Joachim imezidi kukumbwa na majaribu.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kesho Saa 9:30 Alasiri kwa saa za Mauritius Uwanja wa Curepipe mjini Curepipe kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye Dar es Salaam.

Awali, Yanga SC ilipanga kuondoka Jumatano wiki hii, lakini ikaahirisha safari baada ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SA), kushindwa kuwapatia ndege ya kuunganisha mapema mjini Johannesburg, kwenda mjini Curepipe.

Kwa sababu hiyo, Yanga SC ikaachana na SA na kuamua kukodi ndege ya Shirika la Tanzania (ATC) ambayo walitarajiwa kusafiri nayo Alfajiri ya leo, lakini hadi sasa wachezaji wameganda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Sababu ni kwamba, ndege waliyotarajiwa kusafiri nayo imepata dosari kidogo – hivyo kwa sasa inafanyiwa marekebisho na matarajio ni timu hiyo kuondoka kuanzia jioni.

“Tupo Uwanja wa ndege sasa, tunasubiri ndege yetu inafanyiwa marekebisho ndiyo tuondoke,” amesema Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro. Na alipoulizwa wanatarajiwa kuondoka saa ngapi, amejibu: “Mchana hivi kwenye saa nane, au saa tisa (Alasiri).”

Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ameamua kubeba kikosi chake chote kwa safari ya Mauritius, kwani baada ya mchezo huo Jumamosi, ndege hiyo ya ATC itaichukua timu hiyo kuipeleka Pemba, visiwani Zanzibar.

Yanga SC itaweka kambi kisiwani Pemba, kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya mahasimu Simba SC, Februari 20, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mkuu wa Msafara anatarajiwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi, wakati upande wa viongozi wanakwenda Katibu Mkuu, Baraka Deusdedit na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu, Jerry Muro.

error: Content is protected !!