July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Yanga yaja na mikakati ya kuiteka Zambia

Suma Mwaitenda, Mwenyekiti wa kamati ya Hamasa za Yanga

Spread the love

KLABU ya Yanga kupitia kamati ndogo ya hamasa imepanga mikakati ya kusafiri na mashabiki kuelekea kwenye mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zesco utakaochezwa tarehe 28 Septemba, 2019 kwenye Uwanja wa Levi Mwanawasa. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Suma Mwaitenda amesema, kwa sasa wameweka mikakati miwili mikubwa kama kuipa hamasa timu yao kupitia mitandao ya kijamii sambamba na kuratibu safari ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kwenda nchini Zambia kuishangilia timu yao.

“Kama kamati ya hamasa tuna mpango wa kuratibu safari kwa mashabiki na wanachama kwenda kuishabikia timu Ndola, tunaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenda kuisapoti timu yao katika siku hizi chache zilizobaki,” alisema Mwaitenda.

Kamati hiyo pia imeeleza kuwa gharama ya safari hiyo itakuwa Sh. 200,000 kwa nauli ya kwenda na kurudi kwa kila shabiki na utaratibu wote utafanyika kwenye makao makuu ya klabu hiyo.

Yanga ambayo mchezo wa kwanza walilazimishwa sare ya mabao 1-1 inakwenda kurudiana na Zesco United nchini Zambia ambao wanarekodi ya kutopoteza mchezo wowote kwenye uwanja wao wa nyumbani toka mwaka 2012 kwenye michezo ya ligi ya kwao na kimataifa.

Kama Yanga itafanikiwa kushinda mchezo huo itakuwa imefuzu kwenye hatua ya makundi barani Afrika na kama itapoteza mchezo huo watakwenda kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

error: Content is protected !!