January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Yanga yaingia mtegoni Zimbabwe

Wachezaji wa Yanga muda mchache kabla ya kuanza safari la Bulawayo, Zimbabwe kuwavaana Platnum

Spread the love

TIMU ya Yanga inaenda kucheza mechi ya marudiano dhidi ya FC Platnum ya Zimbabwe, lakini akili yao ipo katika mchezo wa raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Etoile du Saleh ya Tunisia na Benifica de Luanda ya Angola.

Hii inaonesha kuwa Yanga wameshaingia kwenye mtego wa Wazimbabwe hao kuwa wameshakubali kutolewa katika michuano hiyo baada ya kukubali kipigo cha mabao 5-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Pia kitendo cha Yanga kwenda Zimbabwe siku mbili kabla ya mchezo wao wa marudiano dhidi ya Platnum ni mtego mwingine katika kuelekea mchezo huo kutokana na hali ya hewa ya Dar es Salaam kuwa tofauti na mji wa Zvishavane utakapochezwa mchezo huo.

Mtego wa kwanza wa Platnum kwa Yanga ulianza mara tu baada ya kumalizika kwa mchezo wa kwanza, wakati kocha wake, Norman Mapeza alipotamka kuwa hawawezi kusonga mbele kutokana na kipigo walichopata.

Platnum wanahitaji ushindi wa mabao 4-0 ili waweze kusonga mbele katika michuano hiyo lakini kauli ya kocha wao inawajengea imani Yanga kuwa wao hawawezi kupata ushindi huo katika mechi yao ya nyumbani

Kauli hiyo ni mtego kwa Yanga ili kuwateka kusaikolojia, wajione wamemaliza kazi katika hatua hiyo, lakini ukweli upo wazi kuwa dakika 90 za mechi ya marudiano ndiyo itakayoamua mshindi wa kuvuka hatua hiyo ya kwanza.

Benchi la ufundi la Yanga, wachezaji na viongozi wanatakiwa kuwafuata Platnum wakijua kuwa wana deni la kushinda katika mchezo huo ili wasonge mbele, lakini wakiingia kwenye mtego wa wapinzani wao, safari yao itaishia katika mji wa Zvishavane, Zimbabwe.

Wapinzani wa Yanga tayari wameanzisha mipango ya kupata ushindi wa mabao mengi katika mchezo huo huo tofauti na kauli zao walizozitoa Dar es Salaam, ambapo kikosi cha Yanga kitalazimika kusaifiri kwa basi umbali wa km 385 kutoka Harare mpaka Zvishavane.

Hali ya hewa katika mji wa Zvishavane ni tofauti na Dar es Salaam, hivyo kuna uwezekano mkubwa hali ya hewa ndiyo sababu ya Platnum kupoteza mechi yao ya ugenini, hivyo wanaweza kupata matokeo mazuri katika mchezo wao wa nyumbani.

Klabu ya Yanga imetoa tarifa mbili tofauti, moja ilidai wanaondoka siku ya Jumatano Aprili 1, 2015 kuelekea nchini Zimbabwe, lakini taarifa ya pili inasema wataondoka Ijumaa ya Aprili 3 mwaka huu, ikiwa siku moja kabla ya mchezo huo utakaochezwa Aprili 4 mwaka huu.

Kama Yanga watakuwa wanaondoka Aprili 3 mwaka huu, watakuwa wameingia katika mtego wa pili kwa Platnum, kwani itakuwa ngumu kwao kuzoea hali ya hewa nchini humo hivyo wanaweza kukubali kipigo cha mabao mengi kama kilichowakuta wapinzano wao.

Wakati Yanga wanajiaminisha kuwa wameshakata tiketi ya kutinga hatua ya pili ya michuano hiyo, wanatakiwa kukumbuka matokeo ya ajabu yaliyotokea kwa wapinzani wao Simba dhidi ya Mufurira Wonderers ya Zambia.

Simba iliwahi kukutana na Mufurira ambapo katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Dar es Salaam, walikubali kipigo cha mabao 4-0, lakini wakiwa ugenini walifanikiwa kushinda mabao 5-0 na kusonga mbele.

Lakini Yanga wanatakiwa kujifunza kwao wao wenyewe katika mchezo wao wa Ligi Kuu Bara msimu dhidi ya Simba uliochezwa Oktoba 20, 2013 uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Katika mchezo huo Yanga walikuwa na uhakika wa kumaliza kwa kushinda mabao mengi, kwani mpaka mapumziko walikuwa mbele kwa mabao 3-0, lakini hali ilibadilika na Simba kushinda mabao matatu katika kipindi cha pili na mchezo huo kumalizika kwa sare.

Mechi ya awali Yanga walifanikiwa kuwaondoa BDF XI ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa awali na kufungwa mabao 2-1 katika mechi ya marudiano.

Yanga walienda katika mchezo wa marudiano wakiwa na lengo la kupata bao la ugenini, lakini baada ya kupata bao hilo waliliridhika na kuruhusu mashambulizi ambayo yaliwapa nafasi wapinzani wao kupata mabao mawili na kufanya mchezo huo kumalizika kwa mabao 2-1.

Mechi ya maruduano ya Yanga na Platnum lolote linaweza kutokea, hivyo Yanga wanatakiwa kujipanga kwa kushinda mchezo huo.

error: Content is protected !!