May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Yanga yafurika kwa Mkapa, burudani kama zote

Spread the love

YES ni siku kubwa. Kilele cha Wiki ya Wananchi. Hakuna ubishi hii ndiyo Yanga Afrika. Mabingwa wa Kihistoria nchini Tanzania. Anaripoti Wiston Josia, TUDARCo … (endelea).

Hivi ndivyo unaweza kuelezea kile ambacho kinaendelea katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ambapo kuna kilele cha sherehe za Wiki ya Mwananchi.

Maelfu ya Wanayanga wameujaza uwanja wa Benjamin Mkapa, wenye uwezo wa kubeba watu 60,000 wakiwa wamekaa.

Tangu asubuhi ya leo Jumapili, tarehe 29 Agosti 2021, nyomi ya mashabiki wa timu hiyo kongwe Afrika, wamejitokeza kuhakikisha wanaweka historia ya kushiriki tukio hilo kubwa na la aina yake.

Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla amesema “haikuwa rahisi kuandaa sherehe hizi. Tunawashukuru mashabiki wetu kwa kutueleza na kujitokeza kwa wingi kama unavyoona.”

Kikosi cha Yanga, kimeingia uwanjani kuwasalimia mashabiki walioujaza uwanja huo, wakiwa wamevalia suti maridadi kabisa.

Burudani mbalimbali zimetolewa na wasanii kama vile Mandy, Madee, Bwax na wengine kibao huku msainii mkubwa Koffie Olomide kutoka Congo akimwaga burudani ya kutosha akiwa amevalia mavazi ya njano kuanzia kofia hadi viatu.

Wakiwa katikati ya uwanja, wachezaji wa Yanga ambao inasaka kurejesha heshima yake ya kunyakua makombe iliyoyakosa kwa misimu minne mfululizo kwa watani zao Simba kunyakua, wameimba wimbo maalum wa timu hiyo wakiongozwa na mlinda mlango wao, Ramadhani Kambwili.

Baadaye kutakuwa na utambulisho wa wachezaji wa timu hiyo pamoja na bechi la ufundi la msimu ujao wa 2021/22. Pia, kutakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Zanaco ya Zambia.

Wachezaji wa Yanga walioitwa timu ya Taifa, wameruhusiwa kuungana na wenzao kwenye tamasha hilo kisha baadaye watarejea kambini.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali.

error: Content is protected !!