May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Yanga: Hatujapokea hukumu ya Mwakalebela

Hassan Bumbuli, Afisa Habari na Mawasiliano wa Yanga

Spread the love

 

KLABU ya Yanga kupitia kwa Afisa Habari na Mawasiliano, Hassan Bumbuli, amesema mpaka sasa hawajapokea nakala ya hukumu ya Makamu Mwenyekiti wao, Frederick Mwakalebela, baada ya kufungiwa kutojihusisha na mpira wa miguu kwa miaka mitano. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea) 

Mwakalebela alifungiwa tarehe 2 Machi, 2021 baada ya kukutwa na hatia katika makosa mawili, ikiwemo kuvishutumu vyombo vinavyosimamia Ligi Kuu Tanzania Bara, kuwa wanahijumu klabu ya Yanga na kushindwa kuthibitisha madai hayo mbele ya Kamati ya Maadili ya TFF.

Akijibu swali wakati wa mkutano wa waandishi wa habari leo, makao makuu ya klabu hiyo, Bumbuli amesema mpaka leo hawajapata nakala ya hukumu licha ya kupokea barua nyingine kutoka TFF, ikitaka kufanya kikao siku ya Jumatatu, hivyo jambo hilo litaongelea baada ya kikao hicho.

“Tumepokea barua nyingine kutoka TFF, ikitaka tufanye kikao siku ya Jumatatu, hivyo haya mambo yote yatazungumzwa baada ya kikao na wenye mamlaka watayazungumzia kwa mapana na marefu,” alisema Bumbuli.

Klabu hiyo hivi karibuni ilikutana na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo pamoja na TFF ili kujadili sintofahamu iliyopo baina ya taasisi hizo mbili kwa siku za hivi karibuni.

Yanga kesho inarejea kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo itashuka uwanjani dhidi ya KMC mchezo utakaopigwa majira ya saa 1 usiku kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jiijini Dar es Salaam.

Kuelekea mchezo huo, Bumbuli amesema wanatarajia kuwakosa wachezaji wanne, ambao ni Mapinduzi Balama pamoja na Yassin Mustapha wote ni majeruhi, Farid Mussa anasumbuliwa na Malaria huku Haruna Niyonzima alichelewa kuripoti kambini hivyo hatokuwa sehemu ya mchezo.

error: Content is protected !!