Sunday , 25 February 2024
Habari MchanganyikoTangulizi

Yametimia

Aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu akisalimiana na Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
Spread the love

UTEUZI uliotabiliwa na Gazeti la MwanaHALISI kuhusu kung’oka kwa aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu umetimia, anaandika Mwandishi Wetu.

Katika andika la Gazeti la MwanaHALISI Desemba 21 la lilieleza nia ya Rais Magufuli kutaka kumuondoa IGP huyo na hatimaye sasa kukabidhiwa nafasi hiyo Simon Sirro, aliyekuwa Kamishna wa Polisi wa Dar es Salaam (RPC).

Isome hii hapa

IGP Mangu kung’oka

Na Charles William,

MwanaHALISI – Desemba 21, 2015.

RAIS na Amiri Jeshi Mkuu, Dk. John Magufuli anajiandaa kufanya mabadiliko makubwa ndani ya Jeshi la Polisi kwa kumuondoa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa mmoja wa maofisa wa Ikulu zinaeleza kuwa Dk. Magufuli sasa anahitaji kuwa na mkuu mpya wa Jeshi hilo huku IGP Mangu akitarajiwa kupewa ubalozi katika mojawapo ya nchi za Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara na Naibu wake Abdurahmani Kaniki akitarajiwa kushushwa ngazi na kuwa mkuu wa polisi katika mkoa mojawapo kanda ya ziwa.

Iwapo Rais Magufuli atabadilisha mkuu wa jeshi hilo, IGP Mangu atakuwa amelitumikia jeshi hilo kwa muda wa miaka miwili tu baada ya kuteuliwa na Rais Kikwete kushika wadhifa huo Desemba 30, 2013 akitokea ofisi ya Polisi wa kimataifa (Interpol) jijini Nairobi, Kenya.

Wanaotajwa kuwa kwenye nafasi ya kumrithi IGP Mangu ni pamoja na mkuu wa Operesheni wa polisi, Simon Siro na mkuu wa Interpol Gustav Babile.

Kwasasa waliopo katika nafasi za juu za jeshi hilo ni kamishna Glodwig Mtweve (fedha na utawala), Mussa Ally Mussa (Polisi Jamii makao makuu), Thobias Andengenye (utawala na utumishi) na Diwani Athumani (Mkuu wa intelijensia ya jinai DCI).

Haya yanakuja ikiwa ni wiki mbili tu tangu Rais Magufuli afanye mabadiliko ya kushitua  akimuhamisha Kamishina wa Operesheni na Mafunzo Paul Chagonja na kumpeleka kuwa mkuu wa jeshi la zimamoto na uokoaji huku mkuu wa idara ya intelijensia Valentino Mlowola akiteuliwa kuwa kaimu mkurugenzi wa TAKUKURU.

MwanaHALISI limetafuta ukweli zaidi kuhusu kufumuliwa kwa jeshi la polisi, lakini baadhi ya maofisa makao makuu hawakuwa tayari kueleza kiundani.

“Wajibu wetu ni kufanya kazi mahali popote kwa mujibu wa sheria za Polisi yakifanywa mabadiliko na Amiri Jeshi Mkuu tutayatii” alieleza kamishina mmoja wa makao makuu ambaye hakutaka kutajwa gazeti kwa madai kuwa si msemaji wa jeshi hilo.

Uchunguzi wa MwanaHALISI umebaini kuwa mabadiliko zaidi yatafanyika hata kwa wakuu wa jeshi la polisi wa Mikoa mbalimbali ambao wana tuhuma za utovu wa nidhamu na maadili akiwemo mkuu wa polisi mkoa wa Mwanza Justus Kamugisha.

Pamoja na tuhuma zingine kamanda Kamugisha anatuhumiwa kumlinda mtuhumiwa wa ujambazi wa kutumia silaha mkoani Mwanza aitwaye Gabriel.

Uchunguzi umebaini kuwa Desemba 15 mwaka huu jeshi la polisi mkoani Mwanza lilipata taarifa za kuwepo kwa mtuhumiwa huyo katika nyumba moja Kirumba, Mwanza huku koplo John Samo na Mkaguzi Makwaza wakitumwa na mkuu wa upepelezi wa Wilaya ya Ilemela kumfuatilia mtuhumiwa huyo wa wa ujambazi.

Hata hivyo wakiwa bado wanamfuatilia mtuhumiwa huyo, katika hali ya kushangaza askari hao walitakiwa kwenda kujieleza kwa RPC Kamugisha tena kwa maandishi ya kwamba, kwanini wanaifuatilia nyumba hiyo na kisha kupewa uhamisho wa kikazi wa haraka.

Koplo Makwazo amehamishiwa Kisiwa cha Ukara, huku koplo Samo akihamishiwa kisiwa cha Ukerewe ili kuvuruga uchunguzi.

RPC Kamugisha pia anazo tuhuma za kutumia madaraka yake vibaya kwa kumnyanyasa askari wake, G. 2751 PC. Japhet Samwel, aliyeumia mkono akiwa kazini ambapo alinyimwa fedha za matibabu na hata ruhusa na hivyo mkono wa askari huyo kuharibika na kupata ulemavu wa kudumu wa mkono huo.

MwanaHALISI limefanya jitihada za kumtafuta kamanda Kamugisha ili ajibu tuhuma zinazomkabili lakini aliomba asiongee kwa madai kuwa yupo katikati ya watu.

Alipotumiwa sms iliyopokelewa na simu yake saa 21:20:11 Jumamosi usiku ikimtaka kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo RPC Kamugisha hakujibu ujumbe huo mpaka saa 22:40:15 usiku ambapo gazeti hili lilikuwa likienda mitamboni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

Habari MchanganyikoTangulizi

25 wafariki dunia katika ajali Arusha

Spread the loveWatu 25 wamefariki dunia papo hapo mkoani Arusha katika ajali...

Habari Mchanganyiko

“Jamii ielimishwe faida za uhifadhi”

Spread the loveWIZARA ya Maliasili na Utalii imesema ili kukabiliana na migongano...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Biteko afuta likizo watumishi Tanesco, bosi Morogoro yamkuta

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dk. Doto...

error: Content is protected !!