July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ya Sumaye yametimia

Frederick Sumaye
Spread the love

“MGOMBEA urais anayetumia kalamu kuchafua wenzake, akiingia madarakani, atatumia risasi kujisafishia njia.”

Hii ni kauli ya Fredrick Sumaye, aliyekuwa waziri mkuu wa Jamhuri. Aliitoa Mei 2005 wakati wa kinyang’anyiro cha kuwania urais ndani ya chama chake.  

Mwaka 2005, wakati Sumaye akitoa kauli hiyo alikuwa mmoja wa waliokuwa wakitafuta kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hakushinda. Aliishia kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Mwisho wa kinyang’anyiro, ni Rais Jakaya Kikwete aliyepitishwa na chama chake kuwania nafasi hiyo.

Sumaye hakutaja jina la yule aliyemtuhumu kutumia vyombo vya habari kuchafua wenzake; na ambaye akiingia madarakani atatumia risasi kusafisha njia.

Naye hakuwahi kuhojiwa wakati huo alipokuwa anatoa kauli hiyo, wala hajahojiwa hadi sasa.

Lakini wiki iliyopita, serikali ya Rais Kikwete, kwa mara nyingine, ilitenda kama ambavyo Sumaye alitahadharisha. Ilipiga marufuku kuchapishwa magazeti mawili ya kila siku – Mtanzania na Mwananchi.   

Kifungo cha magazeti haya, kimekuja miezi 15 baada ya serikali kufungia kwa “muda usiojulikana” gazeti la kila wiki la MwanaHALISI.

Aidha, kifungo hicho kimekuja miezi minane baada ya serikali kufungia vituo viwili vya radio – Radio Imani ya Morogoro na Radio Neema ya Mwanza. Radio hizi mbili zilifungiwa kwa muda wa miezi sita.

Tayari hivi sasa, Radio Imani na Radio Neema zimetoka kifungoni. Zinafanya kazi yake ya umma; ingawa ndani ya mioyo ya wafanyakazi, wamiliki na wasikilizaji, kumejaa hofu. Hawajui watafungiwa tena lini na kwa muda gani.

Magazeti ya Mtanzania na Mwananchi angalau yanajua lini yatamaliza kifungo hiki haramu – siku 14 kwa Mwananchi na siku 90 kwa Mtanzania kutoka 27 Septemba 2013.

Bali kwa MwanaHALISI, hakuna dalili za kulifunguliwa. Kinachoonekana kwa wengi ni kuwa gazeti hili la Mwananchi, lililobeba dhamana ya kuwa kiongozi katika kufichua ufisadi serikalini na kwenye taasisi zake, linatakiwa kufa.   

 Taarifa kutoka kwenye baraza za ofisi ya Msajili wa Magazeti, Assah Mwambene zinasema, “Hata wamiliki wake hawaruhusiwi kuanzisha gazeti jingine.”

Kufungia MwanaHALISI, ni sawa na kuziba bomba la elimu na maarifa ambalo wengi walilitegemea kwa miaka saba ya uhai wake. Gazeti hili limefungiwa bila kutenda kosa lolote – liwe la kitaaluma wala sheria za nchi. 

Kisingizio kilichotumiwa na serikali kuhalalishia kufungia MwanaHALISI, ndiyo hichohicho kimetumika kufungia Mtanzania na Mwananchi. Ndicho kimetumika kufungia Radio Imani na Radio Neema.

Ni tuhuma za jumla kuwa magazeti haya yamekuwa yakikiuka maadili ya uandishi wa habari; kufanya uchochezi na hivyo kukiuka Sheria ya Magazeti, Na. 3 ya mwaka 1976.

Waziri wa habari ambaye siyo mwandishi wa habari, ndiye polisi. Ndiye mwendesha mashtaka wa serikali (DPP). Ndiye jaji.

Ni yeye pekee anayejua chombo fulani kimekiuka maadili. Ndiye anayesikiliza kesi na ndiye anayeamuru gazeti kufutwa, kufungiwa au kusimamishwa kwa muda anaopenda. Hivyo ndivyo sheria ya magazeti inavyoeleza, inavyoelekeza; na ndiyo wanaopenda kuitumia wanavyotaka iwe.

Hakuna mahali popote ambako serikali yaweza kusimama hadharani kutetea uamuzi wake wa kufungia magazeti haya. Haiwezi.

Kungekuwa na kosa, serikali ingeshitaki. Ingekwenda mahakamani. Makosa yangewekwa wazi; siyo kufinyangwa kama ilivyofanya kwa MwanaHALISI; na sasa kwa magazeti haya mawili. Ukweli ungefahamika. Mahakama ingeamua. Anayeshinda na anayeshindwa wangefahamika. Lakini ilichofanya serikali, ni uviziaji wenye nia ya kuficha ukweli.

Serikali haikwenda mahakamani kwa sababu ilijua haina hoja. Ilijua kuwa haki na uhuru wa kujieleza, kupokea na kutoa habari, kama inavyotambuliwa na Katiba, haina vipingamizi vinavyotajwa kwenye Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo wamekuwa wakiitumia kufungia vyombo vya habari.

Walioamuru magazeti kufungiwa, wanajua kuwekwa kwa vipengele vya Haki za Msingi na Wajibu wa Mwanadamu – Bill of Rights – katika Katiba ya Jamhuri, kulibadilisha sheria zote ambazo zinakiuka haki za binadamu.

Mathalani, wale walioamua kufungia MwanaHALISI, wanajua hakukuwa na udhalilishaji au uongo wowote katika habari na makala ambazo zilichapishwa.

Haya ni matokeo ya ubabe wa watawala na woga uliopitiliza wa kuhofia kile ambacho pengine walidhani kiliwekwa kiporo ili kichapishwe baadaye.

Laiti serikali ingejua kilichokuwa kikiandikwa na gazeti hilo ni sehemu ndogo ya kile kilichokuwa kikiachwa, wangewashukuru waandishi wa gazeti na mchapishaji wake.

Matoleo matatu ya mwisho, kabla ya kufungiwa, yalikuwa juu ya madai ya wanasiasa wa upinzani kutishiwa kuuawa; na utekaji na utesaji wa Dk. Steven Ulimboka.

Swali ambalo wengi wanajiuliza ni hili: Inakuwaje Rais Kikwete ambaye kabla ya kuingia madarakani, alikuwa kipenzi cha waandishi wa habari na vyombo vyao, ndiye huyohuyo serikali yake inafungia magazeti?

Inawezekana ni yeye aliyelengwa na Sumaye kuwa akiingia madarakani atatumia risasi kusafisha njia? 

Lakini kuna hili jingine la “Mkuki kwa Nguruwe kwa binadamu mchungu.” Kwa sisi tuliofungiwa miezi 15 iliyopitia, tunajua nani wanashabikia vitendo hivi; na nani analia pamoja nasi.

Kama sote tungesimama pamoja – hata kabla ya MwanaHALISI halijafungiwa – yote haya yasingetokea.

Hayo yamepita. Leo kuna mengine yanayoashiria kuwa kila mchapishaji ataguswa. Ni wakati sasa wa kusema hapana.

Kuna haja ya kukataa ubabe na udhalimu huu. Serikali iliyokwenda mahakamani kwenye mgogoro wake na walimu; na kisha mahakama ikasikiliza hoja za pande mbili na kutoa hukumu, kwa nini inashindwa kutumia mahakama katika suala la magazeti? Inaogopa nini?

Kwa mfano, wakati inafungia MwanaHALISI serikali ilisema “gazeti hili limekuwa likichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.” Hakuna mahali popote ambako serikali imetaja makala hizo.

Wala serikali haijaweza kutaja matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea baada ya makala hizo kuchapishwa.

Tusiruhusu mtu serikalini au kundi la watu kutumia nafasi zao kuua chombo cha habari ambacho ni mdomo wa umma.

Tuna fursa pana ya kupiga kelele – ndani na nje ya nchi –  kupinga ukatili na uvunjaji haki za binadamu. Tuna fursa ya kwenda mahakamani kupinga vitendo vinavyopora uhuru wetu. Tuna haki ya kuelimisha jamii juu ya ukatili wa sheria ambayo serikali haitaki kufuta.

Hatuwezi kusubiri sheria ijifute au wanaoitumia wafe. Tusimame pamoja, kwa njia yoyote ile, na kushinikiza kupatikana kwa haki yetu na kulindwa kwa uhuru wa kila mmoja.

error: Content is protected !!