August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ya mwaka 1970 bora yajirudie

Spread the love

MARA baada ya kupatikana kwa Uhuru wa (Tanganyika) Tanzania Bara mwaka 1961, ilipofika mwaka 1970 serikali iliutangaza mwaka huo kuwa ni wa Elimu ya Watu Wazima, anaandika Michael Sarungi.

Tangazo hilo liliongeza mwitiko wa wananchi wengi kujiunga katika vikundi mbalimbali na kuanza kujifunza kusoma na kuandika.

Mikakati hii ya serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anajua kusoma na kuandika ilisaidia kuongeza idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika hatimaye kuchochea kuharakisha ya maendeleo ya watu.

Mpango huu uliweka mkazo katika kuhakikisha Elimu ya Watu Wazima inamfikia kila raia na ulipokuja mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano (1969-1974) serikali ilichukua jukumu jipya la kuhakikisha kuimarika kwa utekelezaji wa Elimu ya Watu Wazima.

Kufanikiwa huku kwa mpango wa Elimu ya Watu Wazima kulisaidia kufanikiwa kwa mipango mbalimbali ya serikali kama, Mtu ni Afya 1970, Uchaguzi ni Wako 1970, Wakati wa Furaha 1971, Chakula ni Uhai 1975, Kufuta Ujinga 1971-75, Elimu ya Upe kwa lengo la kuharakisha kufuta ujinga, Kuanzishwa kwa vyuo vya maendeleo vya wananchi 1975 na Mpango wa Maendeleo 1964-69 uliolenga kuwakwamua wananchi kiuchumi.

Kufanikiwa kwa mipango hii yote kulisababishwa na nia na utashi wa viongozi waliokuwepo wakati huo kwa kuweza kuwahamasisha wananchi kwa kuwaeleza ukweli na faida ya elimu katika maisha yanaoyo wazunguka na maendeleo yao kwa ujumla.

Hali hiyo ya idadi ya watu wazima kujua kusoma na kuandika kuliperekea nchi kutunukiwa tuzo maalumu na Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, sayansi na utamaduni(UNESCO) kwa kazi nzuri ya kuhamasisha masuala ya elimu nchini.

Hata hivyo baada ya moiongo mingi kupita na nchi kufanikiwa kupunguza idadi ya wananchi wasiojua kusoma na kuandika leo hii idadi ya wananchi wasiojua kusoma na kuandika imeongezeka maradufu mpaka kufikia asilimia 68 kwa nchi nzima.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) inasema watu wasiojua kusoma na kuandika Duniani wamefikia 774 milioni huku hali ikiendelea kuwa mbaya katika bara la afrika.

Ripoti hiyo inaeleza wazi kuwa idadi kubwa ya watu hao wasiojua kusoma na kuandika wengi wao wanaishi katika bara ya Afrika na Asia, na kwamba takwimu hizo zinaonyesha kiwango hicho kimeongezeka wa asilimia nane kuanzia mwaka 1990 hadi leo.

Kwa upande wa Tanzania hadi kufikia mwaka 2002 idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika ilikuwa watu 6.2 milioni. Idadi hiyo ni kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ambao ni sawa na asilimia 31, lakini kwa sasa idadi hiyo imeongezeka na kufikia watu zaidi ya milioni 14 hali ambayo ni ya hatari kwa maendeleo ya taifa.

Wakati kiwango cha watu wazima wasiojua kusoma na kuandika kikiongezeka kwa asilimia nane kuanzia mwaka 1990, taarifa ya utafiti mpya inasema bado kuna watu milioni 774 duniani wasiojua kusoma wala kuandika idadi kubwa ya watu hao wapo katika mabara ya Afrika na Asia.

Ripoti hiyo ya Unesco imetolewa katika wakati ambapo kiwango cha kujua kusoma na kuandika nchini kikitajwa kuporomoka.Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2002 idadi ya Watanzania wasiojua kusoma na kundika ilifikia milioni 6.2.

Pamoja na kuwepo kwa mikakati anayotaja Waziri Kawambwa, hali katika ngazi ya elimu ya msingi haijawa nzuri. Tafiti zinaonyesha kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi bila ya kujua kusoma na kuandika. Cha kushangaza baadhi ya wanafunzi hao wamekuwa wakichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari.

Kwa mfano, Aprili mwaka jana, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilibaini kuwepo kwa wanafunzi wa sekondari 5200 waliokuwa hawajui kusoma na kuandika. Wanafunzi hao walikuwa sehemu ya wahitimu wa darasa la saba mwaka 2011.

Awali mwaka 2010, asasi isiyo ya kiraia ya Twaweza ilitoa ripoti ya utafiti iliyobainisha kuwa kati ya wahitimu watano wa darasa la saba, mmoja hawezi kusoma hadithi ya kiwango cha darasa la pili.

Kwa hali ilivyo sasa hapa nchini kuna haja ya serikali kurudisha mpango wa Elimu ya watu wazima kwani takwimu zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika.

error: Content is protected !!