September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ya Martin Luther king 1968, yashuhudiwa tena 2020 Marekani

Spread the love

MAANDAMANO, vurugu na uharibifu katika kupinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani mwaka 1968, chini ya mwanaharakati Martin Luther King Jr, sasa yanashuhudiwa tena. Inaripoti mitandao ya kimataifa … (endelea).

Baada ya Luther King kuuawa tarehe 4 Aprili 1968, ziliibuka vurugu, maandamano katika miji mbalimbali ya taifa hilo kupinga mauaji hayo, hali ya wasiwasi nayo ilitawala kutoka na hasira pia uharibifu uliokuwa ukifanywa na waandamanaji.

Kifo cha Luther King Marekani kwa kiwango kikubwa kilivuruga amani, sasa kifo cha George Floyd, Mmarekani mweusi mpaka sasa kinatikisa miji 75 ya taifa hilo huku hofu, uharibifu na maandamano vikishika kasi siku hadi siku.

Ni baada ya Polisi wa Mji wa Minnesota kumuua Floyd. Katika taifa hilo, maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi huo yanaendeshwa na wazungu raia wa taifa hilo, uharibifu mkubwa na kuvamiwa kwa maeneo muhimu vinashuhudiwa.

Mwandishi wa habari wa BBC, Nick Bryant kwenye ripoti yake ameandika, kinachoshuhudiwa sasa na ukubwa wake, kinafananishwa na kile kilichotokea mwaka 1968 baada ya Luther King kuuawa.

Nchini humo, waandamanaji wamekaribia viwanja vya Ikulu, wamepiga mawe na mafataki wakishinikiza hatua zichukuliwe kwa polisi waliomuua Floyd.

Pia, kanisa la kihistoria la St. John’s Episcopal linalojulikana kama ‘Kanisa la Rais’ lililopo karibu na Ikulu hiyo, nalo limeharibiwa ikiwa ni pamoja na baadhi ya vitu vyake kuchomwa moto.

Polisi wa kutuliza ghasia na wanausalama wameongeza nguvu kwenye viwanja hivyo. Hata hivyo, idadi kubwa ya waandamanaji wenye hasira imewalazimu kutumia maji ya washa na gesi ya kutoa machozi kutumika ili kuwatawanya.

Polisi wa miji ya New York, Chicago, Philadelphia na Los Angeles, wameamua kutumia risasi za mpira kukabiliana na waandamanaji.

Floyd alikuwa akifanya kazi kama ofisa wa usalama kwenye mgahawa mmoja jijini humo, alikabiliana na mteja mmoja aliyefika hapo akijaribu kununua bidhaa kwa kutumia noti bandia ya Dola 20.

Alipoanza kumkabili, ndipo mvutano ukatokea na katika dakika chache polisi walipofika hapo, kulikuwa na kutoelewana kati ya polisi hao na Floyd. Walimgeuzia kibao.

Katika maandamano hayo, magari ya polisi na mali za serikali katika miji ambayo maandamano yameshika kasi, vimeripotiwa kuharibiwa kwa kiwango kikubwa.

Televisheni ya Mji wa Philadelphia imeonesha namna waandamanaji wanavyopambana na polisi, uharibifu pamoja na uporaji kwenye maduka makubwa. Uporaji huo umefanyika kwa kiwango kikubwa katika miji ya Santa Monica na California.

Polisi katika majimbo wameendesha kamata kamata, tayari watu 4,100 wamekamatwa kwa madai ya uharibifu wengi wao wakiwa wazungu.

Hata hivyo, Gavana wa 41 wa Jiji la Minnesota, Tim Walz amesema, pamoja na waandamanaji kushinikiza polisi hao wachukuliwe hatua, kesi yao itakuwa ngumu.

Amemtaka Mwanasheria Mkuu (AG) wa taifa hilo Keith Ellison, kushirikiana na wawakili wa Mahakama ya Hennepin, Mike Freeman kushirikiana kwenye kesi hiyo. Ellison amekubali ombi hilo.

“Hii kesi sio ya kawaida, kwasababy Floyd ameuawa lakini nani aliyemuua!: huyu amekufa akiwa kwenye mikono ya wana usalama wa Minnesota,” amesema Ellison na kuongeza “kushutumu maafisa wa polisi kwa makosa ya mauaji ni ngumu sana.”

Ijumaa wiki iliyopita, Freeman ametangaza kufungua madai matatu polisi Derek Chauvin, ambaye ndio aliyemgandamiza Floyd kwa goti na kwamba polisi watatu ambao walikuwepo kwenye mazingira yake, hawajashtakiwa.

error: Content is protected !!