July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ya Kikwete yamkumba Magufuli

Spread the love

HOJA nzito, uchunguzi na ufuatiliaji wa vyama vya upinzani uliokuwa unatesa utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, sasa zinaelekezwa kwa Rais John Magufuli, anaandika Faki Sosi.

Rais Magufuli anakumbana na mtikisiko kutoka vyama vya upinzani ambapo sasa anakosolewa kutokana na kushindwa kutenganisha majukumu ya mihimili miwili –Bunge na Serikali-hivyo kusababisha sintofahamu.

Hatua anazochukua ikiwa ni pamoja na kuhamisha matumizi ya fedha jambo ambalo linatajwa kuingilia muhimili mwingine wa Taifa kinyume na taratibu za nchi.

Mjini Dodoma kabla ya kususa Hotuba ya Kasim Majaliwa, Waziri Mkuu; Freeman Mbowe, Kiongozi wa Upinzani Bungeni amesema utawala wa sasa unavunja Katiba ya Jamhuri.

Mbowe ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni katika Ofisi ya Waziri Mkuu amesema, “kitendo cha serikali kuamua kufanya re-allocation ya bajeti bila kupata idhini ya Bunge ni dharau kwa bunge lakini mbaya zaidi ni uvunjaji wa Katiba na Sheria.”

Amefafanua kwamba, ni Bunge la Bajeti kwa mujibu wa ibara ya 63(3)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndio lililo na mamlaka ya kujadili utekelezaji wa kila wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa Bajeti ikiwa ni kujadili na kuidhinisha Bajeti ya Serikali.

“Ikiwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge hazikutosha kutekeleza majukumu ya serikali, kifungu cha 41(1) cha Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015 kinaelekeza kwamba:

“Serikali itawasilisha Bungeni kwa idhini, bajeti ya nyongeza ya fedha zilizotumika ambazo zimezidi kiwango kilichoidhinishwa na Bunge au kwa madhumuni ya kugharamia mahitaji ambayo hayakupangwa.”

Amefafanua kwamba, utaratibu huo unatiliwa nguvu na Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001 ambapo kifungu cha 18 (3) na (4) kinaitaka serikali kupeleka bungeni bajeti ya nyongeza kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge ikiwa fedha zilizoidhinishwa awali hazikutosha.

Lakini utaratibu huo umekuwa ukivunjwa na Serikali ya Rais Magufuli kutokana na kufanya matumizi ya fedha ambazo hazikuidhinishwa na Bunge na kwamba, jambo hilo linaua dhana ya madaraka ya Bunge ya kuisimamia na kuishauri serikali.

Ametoa mfano kwamba, bajeti ya maendeleo iliyokuwa imeidhinishwa na Bunge kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2015/16 ilikuwa ni Sh. 883.8 bilioni ambapo kati ya fedha hizo, fedha za ndani zilikuwa ni Sh. 191.6 bilioni.

“Jambo la kushangaza ni kwamba, hadi kufikia mwezi Machi 2016 wizara ilikuwa imeshapokea kutoka hazina shilingi bilioni 607.4 ikiwa ni fedha za ndani.

“Ukitazama takwimu hizo, utaona kuwa kuna ongezeko la fedha zilizotolewa na hazina hadi kufikia mwezi Machi 2016 ukilinganisha na fedha zilizoidhinishwa na Bunge,” amesema Mbowe.

Amesema tangu kuidhinishwa kwa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, hakuna bajeti ya nyongeza iliyopelekwa bungeni na serikali ili kupata idhini kutokana na matakwa ya Sheria ya Bajeti ya 2015 au sheria ya Fedha ya 2015.

Hivi karibuni Rais Magufuli amekuwa akibadili matumizi ya fedha zilizopangwa na bunge kwa ajili ya shughuli fulani na kuzipeleka kwenye kazi nyingine kinyume na utaratibu wa nchi.

Miongoni mwayo ni fedha za Sherehe za Muungano ambazo sasa zimeelekezwa kwenye upanuzi wa Barabara ya Makongoro – Uwanja wa Ndege wa Mwanza kuanzia eneo la Ghana.

Fedha za Sherehe ya Uhuru ziliamriwa kuelekezwa kwenye upanuzi wa Barabara ya kutoka Mwenge kwenda Moroco jijini Dar es Salaam ambapo upanuzi huo unaendelea.

error: Content is protected !!