July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wyndham yafungua hoteli Tanzania

Hoteli ya Ramada Resort

Spread the love

SHIRIKA la Hoteli la Wyndham, ambalo linaongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya hoteli na moja kati ya vitengo vitatu vya kibiashara vya Kampuni ya Wyndham Worldwide, limefungua hoteli ya Ramada Resort yenye vyumba 139 jijini Dar es Salaam. Anaandika Mwandishi Wetu… (endelea)

Hoteli hiyo inaongeza idadi ya hoteli za shirika hilo barani Afrika. Zingine zipo Morocco, Ghana, Nigeria na Tunisia, na hivyo kuendeleza upanuzi wa hoteli ya Wyndham katika kanda ya Afrika Mashariki.

Dan Ruff- Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa hoteli ya Wyndham katika eneo la Ulaya, Mashariki ya Kati, Afrika na Bahari ya Hindi, amesema hoteli hiyo ni kwanza Afrika kuendeshwa kupitia kitengo cha usimamizi cha kampuni kinachoendelea kukua.

“Ufunguzi wa Ramada Resort jijini Dar es Salaam una umuhimu mkubwa kimkakati kwetu,” amesema Ruff wakati wa ufunguzi rasmi leo.

Amesema, “Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya malazi yenye ubora wa kimataifa katika Afrika Mashariki, pamoja na dhamira yetu ya kuwa karibu na wageni na wateja wetu kupitia upanuzi katika kitengo cha usimamizi wa mali, hii ni hatua muhimu sana katika ukuaji wetu katika kanda hii.”

Ruff ameongeza kuwa, Ramada Resort ya Jijini Dar es Salaam, yenye vifaa vya kipekee na iliyo kwenye eneo lenye mandhari mazuri ya ufukweni, imeweka viwango vipya kwa mahoteli yenye kiwango cha kati nchini.

“Kati ya vyumba 139, vyumba 117 ni vyenye ubora mkubwa na viko mkabala na ufukwe au na bustani, vyumba 21 ni vya kiwango cha hadhi ya juu na chumba kimoja cha hadhi ya ‘presidential suite’,” amesema.

Naye Murtaza Fazal- mmiliki wa Ramada Dar es Salaam, amesema “Ninafurahi kusaini mkataba wa muda mrefu na Wyndham Hotel Group, kampuni yenye hoteli kubwa duniani.”

“Pia najivunia kuwa mwekezaji wa kwanza kuitambulisha Ramada katika soko la Afrika Mashariki. Ninaamini kuwa hii Ramada mpya iliyoko katika ufukwe wa Jangwani itakuwa ni kimbilio la wenyeji na hata watalii wa kimataifa na wageni wa kibiashara, tunajivunia mazingira bora, ubunifu na huduma bora.”

error: Content is protected !!