August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wosia wa Rais Jumbe wabebwa

Spread the love

KAULI ya Alhaj Aboud Jumbe, aliyekuwa Rais wa Zanzibar ya kugoma kuzikwa ‘kifalme’ kama ilivyo kwa viongozi wengine wa kitaifa, imetekelezwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaandika Hamis Mguta.

Taarifa ya Rais Jumbe kutotaka kuzikwa kifalme ilisambazwa kwa haraka jana baada ya kufariki kwake jambo ambalo lilizua mjadala hasa kutokana na wadhifa wa urais aliowahi kuwa nao ndani ya nchi.

Rais Jumbe ambaye alikuwa rais wa awamu ya pili Zanzibar, alifariki jana mchana nyumbani kwake Mji Mwema, Kigamboni jijini Dar es Salaam na kuzikwa leo Migombani, Unguja.

Miongoni mwa wosia wake ni kutotaka kuzikwa kwa taratibu za kiseriali ikiwa ni pamoja na jeneza lake kufunikwa kwa Bendera ya Tanzania, Bendera ya CCM, kupigiwa mizinga pia kubebwa na watu maalum.

“Sitaki bendi, sitaki mizinga, sitaki maombolezo wala lolote lingine lenye hata chembe ya kufuru,” ni sehemu ya wosia wake uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii jana.

Ni kawaida kwa viongozi wa juu taratibu za mazishi yao kuambatana na jeneza kufunikwa kwa bendera ya taifa, kupigiwa mizinga jambo ambalo kwa Rais Jumbe hakulitaka.

Maisha ya Rais Jumbe baada ya kung’olewa urais yamesikitisha wengi, Serikali ya CCM imemdhalilisha vya kutosha, imemtenga na kumpuuza mpaka uhai wake unafika tamati. Ameondoka akijua kwamba, hana thamani.

Hana thamani kwa Wazanzibari wahafidhina, hana thamani kwa wenye maslahi binafsi bara na visiwani pia hana thamani kwa wasiojua thamani yao ndani ya Zanzibar.

Rais Jumbe amezikwa huku akiwa na fundo kwenye moyo wake, ameondoka akiwa anasononeka. Ni kwa kuwa thamani yake kwa Watanzania hususani Wazanzibari imepigwa teke na CCM.

Amewaacha wenye tamaa ya dunia, wanaojali mkono kwenda kinywaji pasi na uhai wa vizazi vyao, amewaacha ‘wababe’ wanaobebwa na vikosi vya kijeshi. Kwao haki si chochote isipokuwa madaraka.

Serikali ya CCM haina cha kujitetea, ndiyo iliyomdhalilisha Rais Jumbe na ndivyo inadhalilisha wale walio na mtazamo chanya na Zanzibar. Manyanyaso ya walio na mtazamo wa Rais Jumbe hayajakoma na hayatokoma.

Kiongozi huyo ndiye aliyekuwa mwasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar muda mfupi baada ya Mapinduzi ya Januari 1964, pia alikuwa mwasisi wa Muungano uliozaa Tanzania na amaefanya kazi kubwa ya kuwafungua macho Wazanzibari.

Historia ya Rais Jumbe visiwani Zanzibar inaumiza kwa wapenda haki. Inatekenya fikra za mabadiliko hususani wakati huu ambao taifa linaelekea kuzama katika sauti ya mtu mmoja.

Udhalili wa CCM kwa Rais Jumbe ulishika hatamu Januari 1984 baada ya Halmashauri Kuu (NEC-CCM), iliyokutana Dodoma kwa dharura na kuafikia kumvua madaraka.

Alivuliwa madaraka ya urais wa Zanzibar, Uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Umakamu wa Rais wa Tanzania na Umakamu Mwenyekiti wa CCM Taifa. Akabaki mtupu.

Rais Jumbe alivuliwa madaaka yote kwa sababu tu alihoji Muungano. Ni jambo ambalo Mwalim Julius Nyerere hakuwa akitaka kuona mjadala wake ukishika hatamu.

Rais Jumbe alikuwa rais wa awamu ya pili Zanzibar. Dhambi kubwa kwake ilikuwa kunyimwa uhuru- kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwake.

 

error: Content is protected !!