July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wizi mtandaoni: Rais Samia anyooshea kidole usajili laini alama za vidole

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan, amehoji kwanini uhalifu na wizi mtandaoni unashamiri, wakati kuna mfumo wa kusajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole, ulioanzishwa kwa ajili ya kudhibiti vitendo hivyo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Samia amehoji hayo leo Jumanne,  tarehe 18 Mei 2021, akifungua Kiwanda cha Ushonaji cha Polisi, Kurasini mkoani Dar es Salaam.

“Kuna mambo huwa yanatushangaza, mfano mtakumbuka kwamba kulikuwa na sheria wote tufanye usajili wa namba za simu na tuweke vidole wote, ili mtu ijulikane nani anatumia namba ipi, pamoja na usajili huo bado vitendo vya utapeli na wizi kupitia mtandao unaendelea  kushamiri,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amehoji; “lakini hatusikii watu wamefikishwa mahakamani kwa ajili hiyo sasa najiuliza ule usajili ulikuwa wa kiini macho au nini.”

Kiongozi huyo wa Tanzania amesema vitendo vya uhalifu mtandaoni vilipaswa kupungua ama kutokomezwa kabisa, kutokana na matumizi ya mfumo huo.

Aidha, Rais Samia ameliagiza Jeshi la Polisi lishirikiane na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na makampuni ya simu kukomesha vitendo hivyo.

“Sababu kama tumesajili vile kila namba inajulikana na kama kuna namba zisizojulikana zinatoelewa na kampuni gani ya simu, naomba mshughulikie hilo kwa kushirikiana na TCRA, taasisi za fedha za umma na binsfsi, pamoja na kampuni za simu kushughulikia hilo,” amesema Rais Samia.

Zoezi la usajili wa laini za simu kwa njia ya alama za vidole (fingerprint), ulianza kutekelezwa Mei 2019.

error: Content is protected !!