August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wizara ya afya yafunga utoaji taarifa za homa ya mgunda

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Spread the love

Wizara ya Afya nchini Tanzania imetangaza kuisha kwa visa vya homa ya mgunda baada ya wagonjwa 17 kupona kabisa huku kukiwa hakuna kisa kipya. Anaripoti Jonas Mushi, Dar es Salaam…(endelea)

Kutokana na hali hiyo leo Ijumaa tarehe 29 Julai, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametangaza kufunga utoaji wa taarifa maalumu kuhusu ugonjwa huo na badala yake utabakia utaratibu wa kawaida wa utoaji taarifa za magonjwa.

“Toka tulipopokea taarifa rasmi za ugonjwa huu (homa ya mgunda) tarehe 7 Julai hakuna mgonjwa mpya, idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kimaabara ni wagonjwa 20 na vifo vinabaki vitatu,” amesema Mwalimu.

Amemongeza kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa aliyelazwa katika kituo cha kutolea huduma za afya na wagonjwa wote 17 wameruhusiwa kwenda nyumbani na wanaendelea na shughuli zao.

“Hii imethibitisha habari za kisayansi kwamba uonjwa huu unatibika kwa antibiotics,” amesema Ummy.
Pia amesema watu 15 waliokaa na wagonjwa wamefuatiliwa na kupimwa na kugundulika kuwa hawana dalili wala maambukizi ya ugonjwa wa mgunda.

“Wataalamu wetu wanaendelea na utafiti wa kina kwa binadamu wanyama na mazingira yanayowazunguka ili kubaini na kuweka mikakati ya kuuthibiti ugonjwa huu nchini,” amesema.

Amesema Waziri Mkuu alielekeza kuweka dawati moja la afya kwa kuhusisha watu wa sekta za afya, mazingira, mifugo, wanyama, kilimo na watu wa maji.

Ummu amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahathari ya ugonjwa huo na kutoa taarifa wanapoona dalili au mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa huo.

“Licha ya kwamba ugonjwa huu ni mara chache kuambukiza kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine ni muhimu watu wakachukua tahadhari kwa kuepuka kutumia maji au vitu vilivyochafuliwa na mkojo wa wanyama na kunywa maji safi na salama au yaliyotibiwa.”

“Wizara inawaomba wananchi kutoa taarifa ya wagonjwa wenye dalili za kuumwa kichwa, uchovu wa mwili, macho kuvilia damu, kukohoa damu, kusikia kichefuchefu na kuharisha. Pale ambapo unaona mtu ana dalili hizi kutoa taarifa katika vituo vya kutolea huduma za afya.”

Aidha amewaagiza Waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanaimarisha na kufufua timu za ufuatiliaji wa magonjwa pia wafuatilie tetesi zozote, “kwenye afya ya jamii hutakii kudharau tetesi yeyote.”

error: Content is protected !!