Thursday , 25 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Wizara, taasisi zaagizwa kujiunga huduma pamoja
Habari Mchanganyiko

Wizara, taasisi zaagizwa kujiunga huduma pamoja

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi za Serikali ambazo hazijaanza kutoa huduma kupitia vituo vya huduma pamoja vya Shirika la Posta Tanzania zijipange na zihakikishe zinaanza kutoa huduma katika vituo hivyo ndani ya mwaka huu wa fedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Aidha, Majaliwa ameitaka Wizara ya Fedha kupitia madeni ya wadaiwa wote ili kuhakikisha wanalipa madeni yao jambo ambalo litaimarisha shirika hilo.

Amezitaja baadhi ya taasisi hizo ni Tume ya Ajira, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumatatu, tarehe 6 Septemba 2021, wakati akizindia Vituo vya Huduma Pamoja vya Shirika la Posta Tanzania kwenye viwanja vya Posta Makao Makuu jijini Dar es Salaam. Huduma Pamoja ni vituo vitakavyotoa huduma zote za Serikali katika eneo moja kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Taasisi ambazo tayari zimeanza kutoa huduma kupitia vituo hivyo ni RITA, UHAMIAJI, NIDA, BRELA, TRA, PSSSF, NSSF na Halmashauri za Majiji, hivyo Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kupata huduma ambapo kwa sasa huduma hizo zinatolewa katika vituo vilivyopo kwenye ofisi za Posta za Dar es Salaam na Dodoma.

Amesema Serikali itahakikisha miundombinu ya mawasiliano inaboreshwa, wigo wa upatikanaji wa huduma za mtandao wa intaneti kwa gharama nafuu unaongezeka ili wananchi waweze kujiendeleza na kufanya biashara kwa ustawi wa maisha yao. Hivyo Waziri Mkuu amewasihi watumishi wa shirika hilo kufanyakazi kwa welezi na uaminifu mkubwa.

“Uzinduzi wa mradi huu wa huduma za pamoja ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan yenye kuakisi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020. Lengo la Serikali ni kuona mchango wa sekta ya habari na mawasiliano kwenye uchumi unaongezeka sambamba na kutengeneza ajira kwa Watanzania.”

Amesema kuanzishwa kwa mradi huo ni mageuzi makubwa kwa Shirika la Posta Tanzania ambalo lina ofisi 350 nchini na kwamba hiyo ni hatua muhimu itakayondoa usumbufu na kupunguza gharama kwa wananchi kwani hawatolazimika kutembea maeneo mengi tofauti kufuata huduma moja.

Naye, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa sh.3.9 bilioni kwa ajili ya maboresho ya shirika hilo kwa mfumo wa kidijitali. “Tumepokea fedha hizo na bado tutapokea bilioni 3.9 fedha hizi hazina posho wala semina, zote zinakwenda kuboresha mfumo wa shirika hilo na kuwa wa kidijitali.”

Awali, Kaimu Posta Masta Mkuu, Macrice Mbodo alisema mradi huo wa vituo vya huduma pamoja ni sehemu ya miradi ya Tanzania ya kidijitali ambapo katika mradi huo Serikali imetenga jumla ya Dola za Marekani 21,500,000 sawa na Sh. 49.53 bilioni.

Alisema utekelezaji wa mradi huo umegawanyika katika awamu kuu tatu ambapo awamu ya kwanza itahusisha vituo 10 navyo ni Dar es Salaam (Posta Kuu-GPO), Dodoma (Posta Kuu), Arusha (Posta Kuu), Mbeya (Posta Kuu), Morogoro (Posta Kuu), Mwanza (Posta Kuu), Tanga (Posta Kuu), Kigoma (Posta Kuu), Mjini Magharib (Posta Kijangwani) na Kaskazini Pemba (Chake Chake).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

THRDC yaongeza mkataba wa ushirikiano na ABA

Spread the love  MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),...

Habari Mchanganyiko

Rufaa ya Equity Benki, State Oil yakwama

Spread the loveMAHAKAMA ya Rufani, jijini Dar es Salaam, imeshindwa kuendelea na...

Habari Mchanganyiko

Bodaboda waeleza mafanikio mafunzo usalama barabarani

Spread the loveMADEREVA bodaboda katika Jiji la Dodoma wameeleza jinsi mafunzo ya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yaahidi kuendelea kuunga mkono Serikali za Mitaa

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya...

error: Content is protected !!