Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wizara Nishati yajivunia mafanikio lukuki 2015-2020
Habari za Siasa

Wizara Nishati yajivunia mafanikio lukuki 2015-2020

Dk. Medard Kalemani, Waziri wa Nishati
Spread the love

WIZARA ya Nishati na Madini imeeleza mafanikio yake kwa kipindi cha miaka mitano (2015-2020). Anaandika Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).  

Katika hotuba ya wizara yake, Dk. Medard Matogolo Kalemani, waziri wa wizara hiyo bungeni jijini Dodoma leo tarehe 8 Mei 2020, ameeleza kwamba, katika sekta hiyo imepata mafanikio makubwa.

Akiorodhesha mafanikio hayo Dk. Kalemani amesema, kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa umeme na kwamba hadi kufikia mwezi Aprili 2020, uwezo wa mitambo ya kufua umeme nchini umeongezeka na kufikia jumla ya MW 1,601.84 kutoka MW 1,308 mwaka 2015 sambamba na kukamilika kwa miradi ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I MW 150 na Kinyerezi II MW 240.

“Ujenzi wa miradi ulikamilika kwa asilimia 100 mwaka 2016 na mwaka 2018 mtawalia, ambapo jumla ya MW 398.22 zimeingizwa kwenye Gridi ya Taifa,” amesema.

Amesema, kuna muendelezo wa ujenzi wa mradi wa Julius Nyerere Hydro Power Project (JNHPP) MW 2,115), ambao hadi sasa utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 85.

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuendelea na utekelezaji wa mradi wa Rusumo MW 80, ambao hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 61.

Wizara hiyo imeeleza kuwa, imefanikiwa kuunganisha Mikoa ya Lindi, Mtwara, Njombe na Ruvuma katika Gridi ya Taifa, ambako kumewezesha kusitisha uzalishaji wa umeme kwa kutumia mitambo ya mafuta mazito ambayo ilikuwa ikigharimu wastani wa Sh. 15.3 bilioni kwa mwaka.

“Kuendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 220 kwa ajili ya Mradi wa Treni ya Mwendo Kasi (SGR), awamu ya kwanza (Lot I) yenye urefu wa kilomita 160 kutoka Dar es Salaam hadi Kingolwira, Morogoro.

“Kuendelea na utekelezaji wa mpango kabambe wa kusambaza umeme vijijini ambapo hadi kufikia mwezi Aprili, 2020 jumla ya vijiji 9,112 vimeunganishiwa umeme ikilinganishwa na vijiji 2,018 vilivyokuwa vimeunganishwa umeme mwaka 2015.

Amesema, wizara imefanikiwa kuendelea kutokuwa na mgawo wa umeme nchini na kuwa na ziada ya umeme wa wastani wa MW 325 kwa siku.

Na kwamba, kumekuwa na muendelezo wa uzalishaji wa vifaa vya kujenga miradi ya umeme nchini, hivyo kusitisha uingizaji wa vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya umeme ikiwemo nguzo, mashineumba, nyaya na mita za LUKU ndani ya nchi na hivyo kurahisisha upatikanaji wa vifaa hivyo.

Miongoni mwa mafanikio Dk. Kalemani amesema, wateja wapya 1,293,528 wameunganishwa na umeme na kufanya jumla ya wateja waliounganishiwa umeme hadi mwezi Aprili, 2020 kufikia 2,766,745, ikilinganishwa na wateja 1,473,217 waliokuwepo hadi Juni 2015 sawa na ongezeko la asilimia 88.

Wizara hiyo imeeleza, kumekuwa na ongezeko la kiwango cha upatikanaji wa umeme (Overall Electricity Access rate) nchini, kutoka asilimia 67.8 mwaka 2016 na kufikia asilimia 84.6 mwaka 2020.

“Serikali kupitia TANESCO na Mpango wa Kupeleka Umeme Vijijini (REA), kuendelea kuunganisha umeme kwa Sh. 27,000 katika maeneo yote ya vijijini.

“Serikali imeongeza kwa gesi asilia iliyogunduliwa kutoka futi za ujazo trilioni 55.27 mwaka 2015 na kufikia futi za ujazo trilioni 57.54 mwaka 2020, sawa na ongezeko la futi za ujazo trilioni 2.27,” ameeleza.

Mafanikio mengine ni kwamba, amesema wizara hiyo imeimarisha shughuli za kaguzi za gharama katika Mikataba ya PSAs (PSA Audit), na hivyo kuokoa Sh. 10.14 bilioni kwa kaguzi zilizofanyika kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2016 hadi 2018.

Pia kumekuwepo na uanzwaji wa shughuli za utafutaji wa mafuta katika Kitalu cha Eyasi Wembere, ambapo visima vifupi viwili (2) vyenye kina cha urefu wa mita 300 vimechorongwa katika Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora na Meatu Mkoani Shinyanga.

Amesema, “Kasi ya usambazaji wa gesi asilia imeongezeka ambapo katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Mtwara, jumla ya nyumba za wateja wa awali zaidi ya 1,000 zimefikishiwa miundombinu ya usambazaji gesi asilia na viwanda 48 vimeunganishwa kufikia mwezi Aprili, 2020.

“Aidha, zaidi ya magari 400 yamefungwa mifumo ya matumizi ya gesi asilia ikilinganishwa na magari 60 yaliyokuwa yameunganishwa mwaka 2015.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!