January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali kuwapiga faini wanaobadilisha matumizi ya ardhi

Spread the love

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini imewataka wamiliki waliobadili matumizi ya ardhi kinyume cha sheria wakalipe faini ikiwa ni pamoja na kupata kibali cha kuendesha shughuli hiyo vinginevyo watachukuliwa hatua. Anaandika Sarafina Lidwino.

Wizara hiyo imepanga kuanza ukaguzi wa maeneo yote nchi tarehe 8 Februari mwaka huu na kwamba, zoezi hilo litaenda sambamba na utozwaji faini kwa wamiliki wa nyumba zisizolipiwa kodi ambapo mkakati huo utatekelezwa kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 na sheria ya mipango miji namba 8 ya mwaka 2007.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Denis Rugemalila, Mkuu wa Kitengo cha Kodi amesema, kuna baadhi ya waendelezaji wa ardhi wamekuwa wakibadili matumizi ya ardhi bila kibali na hivyo kusababisha kero kwa wakazi wa maeneo husika.

“Kwa mfano mtu anaomba kibali kwa ajili ya makazi ya nyumba moja lakini matokeo yake anajenga saba na wakati mwingine anafanya biashara huku analipia kodi ya makazi tu. Hadi sasa tumebaini nyumba 2000 zisizolipa kodi na zoezi bado linaendelea,” amesema Rugemalila.

Amesema kuna tatizo kwa baadhi ya waendelezaji wa ardhi la kutoacha nafasi kwa ajili ya matumizi ya umma kama inavyotakiwa na kwamba ni ukiukwaji wa makusudi wa sheria ya mipango miji namba 8 ya 2007.

“Zoezi hilo tutalifanya kwa kushirikiana na Manispaa za Halmashauri zote ambapo tumetoa siku 14 kuanzia Februari 8 kila mmiliki asiyelipa kodi ya pango alipe kwa hiari na baada ya hapo atachukuliwa hatua,” amesema Rugemalila.

error: Content is protected !!