August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wiraza ya Ardhi kutibu migogoro ya ardhi

Spread the love

WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza mchakato wa kupitia sera ya ardhi ya mwaka 1995 ili kuangalia upungufu uliopo ikiwemo tatizo la migogoro ya ardhi na hatimaye kuandaa sera mpya ya ardhi itakayondoa changamoto zote, anaandika Christina Raphael.

Katika mchakato huo,wizara hiyo imekutanisha wadau mbalimbali ambao wanafanya mapitio ya sera hiyo kwa kupitia kila kipengele na kubaini changamoto zake pia kujadili kwa pamoja namna ya kuboresha ili kuweza kuleta tija.

Wadau hao ni pamoja na wakuu wa wilaya, wenyeviti wa halmashauri, maofisa ardhi wa halmashari na mikoa, wawakilishi wa wakulima na wafugaji, mitandao inayounganisha wakulima, taasisi na mashirika yanayoshughulika na kilimo na ufugaji, wawakilishi wa wavuvi na wachimba madini.

Akizungumza kwenye mkutano wa wadau hao Dk. Adam Nyaruhuma, mwezeshaji kutoka wizarani amesema, hatua hiyo inatokana na sera ya ardhi iliyopo sasa imepitwa na wakati.

Amesema kuwa, wadau hao wataipitia sera hiyo ya mwaka 1995 vipengele muhimu na kutoa maoni yao hususani kwenye mifumo ya kumiliki ardhi, haki ya mwanamke kumiliki ardhi, utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye mabaraza ya ardhi, mamlaka ya rais kubadilisha umuliki wa ardhi na namna ya kupata madini yaliyopo kwenye ardhi inayomilikiwa.

Kikando Abaro, mwakilishi wa wafugaji amesema kuwa, anaungana na serikali kupitia wizara hiyo katika kupitia upya sera ya ardhi ya mwaka 1995 ili iweze kutengenezwa sera mpya itakayokidhi matakwa ya kila mtu anayemiliki ardhi kwa matumizi yake.

Amesema kuwa, ni vyema sera hiyo mpya isaidie namna gani mfugaji anaweza kumiliki ardhi kulingana na mifugo yake ili kupunguza tatizo la wafugaji kuhamahama kwani ndio limekuwa likichangia migogoro ya wakulima na wafugaji.

Mukhusini Omary, Mwenyekiti wa Ushirika wa Wakulima wa Bonde la Mgongola wilayani Mvomero amesema, pamoja na jitihada za wizara na serikali kuboresha sera ya ardhi lakini bado wakulima wengi hawaifahamu sera hiyo.

“Mimi nilivyoitwa katika mkutano huu ndio nimeona sera hiyo ya mwaka 1995 baada ya kupewa kitabu, inafika mahala hata hujui utoe maoni gani, mi nadhani kwanza ingetolewa elimu kwa wakulima na wafugaji kuijua vizuri hii sera na baadaye ndio wapewe nafasi ya kuchangia katika kuiboresha,” amesema Omary.

Awali akifungua mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Luacas Mwaisaka, Katibu Tawala Msaidizi Huduma za Miundombinu amesema sekta ya ardhi imevamiwa na madalali na hali hiyo ni sababu kubwa ya kuwepo kwa migogoro ya ardhi ikiwemo ile iliyopo mkoani hapa.

error: Content is protected !!