August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wimbo wa ‘Dikteta Uchwara’ waponza wawili

Spread the love

WATU wawili akiwemo Fulgency Mapunda ‘Mwanakotide’ (32, mwanamuziki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakituhumiwa kumuudhi Rais John Magufuli, kupitia wimbo unaojulikana kama Dikteta Uchwara, anaandika Faki Sosi.

Wimbo wa ‘Dikteta uchwara’ uliotungwa na Mapunda na kurekodiwa na Mnesa Sikabwe (39), ambaye ni mtayarishaji wa muziki, unapatikana katika mtandao wa YouTube. Inadaiwa kuwa maudhui yake yalilenga kumuudhi Rais Magufuli na hivyo watu hao wawili kushitakiwa. 

Mapunda na Sibakwe wanashitakiwa kwa kosa moja. Dereck Mkabatunzi, wakili wa serikali, mbele ya Thomas Simba, Hakimu Mkazi Mkuu, katika mahakama hiyo amesema, watuhumiwa wanakabaliwa na kosa la kusambaza taarifa zenye lengo la kumuudhi Rais Magufuli.

Wanatuhumiwa kutenda kosa hilo katika tarehe tofauti, kati ya Agosti, mwaka huu maeneo ya Manzese jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa, washitakiwa hao kupitia mtandao wa YouTube kwa makusudi, walisambaza wimbo uliopewa jina la ‘Dikteta Uchwara’ ambao umebeba maudhui ya kumdhalilisha na kumuudhi Rais Magufuli.

Watuhumiwa wamekana kosa hilo huku wakili wa serikali, Mkabatunzi, akieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kwamba hakuna pingamizi na dhamana.

Mapunda na Sibakwe wamedhaminiwa na wadhamini wawili, waliosaini bondi ya Sh. 10 millioni na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 12, mwaka huu.

error: Content is protected !!