July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Wilaya fuateni muongozo kuhusu Udiwani’

Spread the love

VIONGOZI wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wa ngazi ya wilaya wamehimizwa kutekeleza maamuzi yaliyofikiwa na viongozi wao wakuu kuhusu utaratibu wa kusimamisha wagombea udiwani ili kuepusha migongano isiyo lazima. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia amesema yeye na wenyeviti wenzake hawatarajii kusikia viongozi wenzao wa vyama hivyo ngazi ya wilaya wanavutana katika kugawana Kata wakati muongozo umetolewa.

Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi ametoa kauli hiyo kama hatua ya kuzima mivutano iliyoanza kujitokeza kwenye wilaya ambako tayari majimbo yote ya uchaguzi yameshafanyiwa uamuzi wa chama kipi kinawakilisha kugombea ubunge.

Amesema baada ya maafikiano ya kugawa majimbo kwa ngazi ya uchaguzi wa ubunge, msimamo wa viongozi wakuu ni kwamba kwa suala la udiwani, watazingatia ni chama kipi kilichopata haki ya kuwakilisha katika uchaguzi.

“Viongozi wetu ngazi ya wilaya ni lazima watekeleze maamuzi tuliyokubalina. Wakati wa kampeni tutawapigia kampeni wagombea kutoka vyama tulivyokubaliana na kwa kuzingatia muongozo tulioutoa kuhusu uchaguzi ndani ya Kata,” amesema Mbatia.

Agosti 13, makatibu wakuu wa vyama vya UKAWA walisoma muongozo mbele ya waandishi wa habari usemao kwamba ni muhimu katika kata vyama vishirikiane kuweka mgombea mmoja kama ilivyofanyika kwa ubunge na urais.

Muongozo huo umeelekeza kwamba vigezo vya kutumika katika kusimamisha mgombea udiwani katika kata, ni pamoja na matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na chama kinachoshikilia kata husika kutokana na uchaguzi uliofanyika.

Vigezo vingine ni idadi ya kura ambazo chama mshirika wa UKAWA kilipata kwa pale ilipotokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndio mshindi kwa uchaguzi uliopita; matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014; mtandao wa chama katika Kata husika; mila, desturi na utamaduni wa jimbo au kata husika, na mgombea anayekubalika katika jamii.

Pamoja na vigezo hivyo, makatibu wakuu walihimiza kuwa viongozi wa wilaya na walio chini yao watumie njia ya ushirikiano na maridhiano kufikia muafaka wa chama kipi kiachiwe kutoa mgombea udiwani kwenye kata.

Imehimizwa pia kwamba viongozi wahakikishe kuwa mtu anayeteuliwa asiwe tu anayekubalika, bali asiwe na kashfa inayoweza kuwachukiza wananchi na kuamua kutomchagua hata kama wanaamini katika vyama vya UKAWA.

Muongozo ulisomwa katika mkutano uliohudhuriwa na vyama vyote vya Chadema, Chama cha Wananchi, NCCR-Mageuzi na Nationakl League for Democracy (NLD). Viongozi waliowakilisha vyama hivyo, ni Dk. George Kahangwa (NCCR-Mageuzi), John Mnyika (Chadema), Tozzy Matwanga (NLD) na Magdalena Sakaya (CUF).

error: Content is protected !!