July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wezi waitia hasara ya 720.5 Mil Tanesco

Spread the love

WIZI wa umeme unaofanywa na baadhi ya watu katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani umeitia hasara ya Sh. 720.5 milioni Shirika la Umeme nchini, anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza na MwanaHalisi Online, ofisini kwake jijini Dar es salaam leo, Adrian Severin, Ofisa Uhusiano wa Tanesco amesema, wamebaini hasara hiyo katika kampeni endelevu inayokwenda kwa jina la Operesheni Kamata Wezi wa Umeme (KAWEU).

“Tangu kuanza kwa kampeni endelevu ya Operesheni Kamata Wezi wa Umeme, Desemba mosi mwaka jana, shirika limebaini kupoteza kiasi cha shilingi milioni 720.5 kutokana na wizi wa umeme katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani,” amesema Severin.

Severin amesema kuwa, Tanesco iliwakamata wateja 252 wanaoshutumiwa kwa makosa mbalimbali,kati ya wateja 14,996 waliokaguliwa Desemba 2015 hadi mwishoni mwa Januari mwaka huu.

Wateja waliokamatwa ni sawa na asilimia 1.6 ya wateja wote waliokaguliwa kutoka maeneo ya mikoa hiyo, ambayo ni Kinondoni Kaskazini, Kinondoni Kusini, Ilala, Temeke na Pwani.

Severin amesema, wateja hao waligundilika kuwekewa umeme kinyume cha utaratibu na kwamba, shirika limewataka kulipa kiasi cha fedha wanachodaiwa.

“Shirika limewataka wateja hao kulipa kiasi cha fedha wanachodaiwa, hadi sasa pesa ambazo zimelipwa na baadhi ya wateja waliokamatwa kwa makosa ya wizi wa umeme ni Tsh 51.3 milioni,” amesema Severin na kuongeza.

“Wateja wanaoongoza kwa wizi wa umeme waliokamatwa ni Baa maarufu jijini Dar es salaam, Nyumba za Kulala wageni na Klabu za Usiku.”

Shirika limewataka wananchi kuacha kujiunganishia umeme kinyume cha sheria ili kuepuka ajali zinazosababishwa na hitilafu za umeme pia kuharibu miundombinu.

“Shirika linapokosa mapato ya kutosha linashindwa kutoa huduma bora kwenye baadhi ya sehemu zisizokuwa na nishati ya umeme, pia wizi wa umeme na uunganishaji umeme holela unachangia uharibifu wa miundombinu,” amesema Severin.

error: Content is protected !!