TAASISI ya vyombo vya Habari kusini mwa Afrika (MISA-TAN) kwa kushirikiana na wadau wa Habari wameshauriwa kuijengea uwezo jamii katika suala la uhuru wa kujieleza hasa watu wenye ulemavu ili kuongeza uchechemuzi na kuleta maana halisi ya kujieleza. Anaripoti Christina Haule, Dodoma … (endelea).
Akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa hali ya uchechemuzi ya uhuru wa kujieleza katika kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa MISA-TAN mmoja wa watu wenye ulemavu Wakili msomi Gideon Mandese alisema Tanzania ina watu wengi wenye ulemavu wa aina mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine wanapaswa kutambua umuhimu wa kuwa huru katika kujieleza ili kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Alisema waandishi wa Habari wamekuwa wakitumia nafasi yao katika kuibua na kuandika changamoto mbalimbali za watu wenye ulemavu wakiwemo watu wenye Ualbino na kusaidia changamoto ya madhara matukio ya ukatili dhidi yao kupungua au kuisha kabisa.
‘’Kuna kipindi nchi yetu ilichafuka kwa sababu ya mauaji ya watu wenye Ualbino,waandishi waliibua tatizo nakumbuka bungeni aliyekuwa Waziri mkuu Pinda hadi alilia bungeni,matukio yale yalichafua nchi baadae yalikomeshwa lakini mwisho wake haukuripotiwa ili dunia ijue” alisema wakili huyo msomi.
Hivyo aliwaasa wanahabari kujenga tabia ya kueleza mambo mwanzo hadi mwisho ili kuonesha thamani ya uhuru wa kujieleza inavyoweza kufanya kazi katika kuleta manufaa na maendeleo katika nchi.
Naye mwandishi Mwandamizi Edwin Soko aliyeshiriki mkutano huo aliwataka wadau wa Habari kutambua kuwa masuala ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa Habari ni masuala mtambuka kwa jamii yote.
Awali akifungua mkutano huo Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alisema kwa sasa Serikali inaendelea na jitihada za kufanya marekebisho ya sheria ya huduma za Habari ambayo itasaidia wanahabari kufanya kazi zao kwa weledi na kwa kuzingatia maadili.
Leave a comment