July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wenje, Nyerere waivuruga CCM Mwanza

Spread the love

MGOMBEA Ubunge wa jimbo la Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema), amesema Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imechangia kuiuwa elimu na imeshindwa kutafuta mbinu na mikakati ya kuikomboa isiangamie. Anaandika Moses Meseti, Mwanza … (endelea).

Kauli hiyo aliitoa juzi wakati wa mkutano wa hadhara, uliofanyika katika viwanja vya Bendera Tatu, Kata ya Bugarika, Nyamagana jijini hapa na kuhudhuliwa na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, Vicent Nyerere.

Wenje ambaye pia ni Waziri kivuli wa Mambo ya Ndani, amesema kuwa kitendo cha serikali ya CCM kuendelea kushusha madaraja ya ufaulu kuanzia elimu ya msingi na sekondari imesababisha Taifa kuendelea kushuka kielimu.

Amesema kuwa CCM wanafanya kitendo hicho kwa manufaa yao binafsi na kuamini ndiyo itakuwa msaada katika safari yao ya kisiasa ili kuwaaminisha watanzania elimu inayotolewa ni bora kumbe ni chanzo cha kuongeza ujinga kwa watoto wa masikini.

Hata hivyo amesema watanzania wanapaswa kuwapa kura za ndiyo wagombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akiwamo, Edward Lowassa ili kuboresha mitaara ya elimu nchini, na kuondoa ada za shule kuanzia `vidudu` hadi chuo kikuu.

Mgombea ubunge Jimbo la Musoma Mjini, Vicent Nyerere (Chadema) amewataka watanzania kupuuza propaganda za CCM za kuwadanya kuwa, mgombea Urais kupitia Chadema, Edward Lowassa ni mgonjwa kwani sio sehemu ya wabeba vyuma na watunisha misuri.

“Kazi ya hao wenzetu CCM ni uongo na aibu ya kushindwa uchaguzi huu ndo inayowasumbua na sasa wamekosa hoja wameanza kuongea bila mpangilio na kuwaeleza watanzania watawafanyia nini kazi yao ni kuwapuuza,” amesema Nyerere.

Nyerere ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, amesema ni wakati wa mabadiliko kwa kuwa watanzania walishachoka na ahadi za uongo zisizotekelezeka na kusababisha watanzania kuendelea kuishi maisha ya duni.

Mmoja wa wananchi waliohudhulia mkutano huo, Edward Madale, amesema kutokana na CCM kushindwa kuwatekelezea na kutatua kero zao umefika wakati muafaka wa kuacha kukichagua.

error: Content is protected !!