Kikao hicho cha kujadili hatma ya kuipa fedha za mkopo Serikali ya Tanzania, zaidi ya Dola za Marekani milioni 500, kilipangwa kufanyika leo tarehe 28 Januari 2020, lakini kimeahirishwa baada ya WB kufanya kikao cha dharura na wanaharakati pia asasi za kiraia nchini.
Katika barua ya Zitto kwa WB, aliitaka taasisi hiyo kutotoa fedha hizo, zilizopangwa kuboresha sekta ya elimu nchini kwa madai, serikali ya Rais John Magufuli, imeshindwa kuheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu pamoja na kuzuia wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, kuendelea na masomo.
“Mkopo wa Benki ya Dunia utalipwa na kila Mtanzania. Serikali lazima iweke mazingira ya watoto wa kike kupata elimu bila kubaguliwa.
“Watoto waliopata uja uzito shuleni, wawe na fursa kurejea shuleni bila bugudha wala unyanyapaa. Badala ya kulia lia, rekebisheni mkataba wa mkopo,” aliandika Zitto kupitia ukurasa wake wa twitter tarehe 26 Januari 2020.
Kwa mujibu wa mtandao wa CNN, katika kikao hicho cha dharura WB, mjumbe mmoja wa bodi hiyo aliomba kikao hicho kiahirishwe.
Wiki iliyopita, WB ilitoa taarifa kwamba, itafanya kikao cha kujadili sababu zilizotolewa na wanaharakati hao, juu ya kutoipa mkopo huo serikali ya Tanzania.
Miongoni mwa sababu zilizotolewa na wanaharakati hao, ni wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, kuzuiwa kuendelea na masomo kinyume na haki za binadamu, pamoja na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu na utawala bora.
Licha ya tuhuma zinazoelekezwa kwa Rais Magufuli, Bella Bird, Mkurugenzi Mkazi wa WB nchini Tanzania ambaye anatarajiwa kuachia ofisi hiyo Ijumaa wiki hii, kwenye kikao hicho cha dharura aliwaeleza wanaharakati hao sababu za timu yake kupendekeza mkopo huo utolewe.
Leave a comment