October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wazungu waimwagia Taliban matrilioni

Dola za Marekani

Spread the love

 

SIKU chache baada ya uongozi wa kikundi cha wanamgambo wa Taliban walioshika madaraka nchini Afghanistan kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na maofisa wa Serikali ya Marekani na Ulaya,  Umoja wa Ulaya umeridhia kutoa kiasi cha Euro bilioni moja sawa na Sh trilioni 2.6 kwenda Afganistan. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hata hivyo, imeelezwa kuwa fedha hizo zitapelekwa moja kwa moja kwa wananchi na sio kwa viongozi wa Taliban ambao hawatambuliwi na Umoja huo.

Viongozi wa nchi tajiri kiviwanda na zile zinazoinukia kiuchumi wa kundi la G20 wamekutana leo tarehe 13 Oktoba, 2021 kwenye mkutano maalum wa kilele unaofanyika kwa njia ya mtandao, kujadili mgogoro wa kibinadamu unaojitokeza huko Afghanistan.

Rais wa Marekani, Joe Biden na Waziri mkuu wa India, Narendra Modi ni miongoni mwa walioshiriki mkutano huo unaoongozwa na Italia ingawa rais wa China, Xi Jinping na mwenzake wa Urusi, Vladmir Putin waliwatuma wawakilishi wao.

Wakati mkutano huo ulipofunguliwa Mkuu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen alitangaza msaada unaotolewa na jumuiya hiyo kwa ajili ya kuepusha janga kubwa la kibinadamu na matatizo ya kijamii na kiuchumi nchini Afghanistan.

Fedha zilizotolewa na Umoja huo zinajumuisha Sh bilioni 666 kati Sh bilioni 800 ambazo awali zilitolewa na Umoja huo kwa ajili ya kusimamia mahitaji ya dharura ya kibinadamu huku nyingine zilizobakia zikipelekwa kwa nchi jirani na Afghanistan ambazo zimekuwa zikiwakaribisha raia wa Afghanistan wanaowakimbia Taliban.

Taarifa ya Umoja wa Ulaya iliyotolewa leo imesisitiza kwamba fedha zake zinakusudiwa kuwafikia moja kwa moja waafghanistan na kuwapa msaada wa moja kwa moja ambapo zitafikishwa kupitia mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi ndani ya Afghanistan na wala hazitokwenda kwa serikali ya mpito ya Taliban ambayo Umoja wa huo wa Ulaya mjini Brussels hauitambui.

Ikumbukwe kwamba msaada wa maendeleo unaotolewa na Umoja wa Ulaya ni tofauti na msaada wa kibinadamu na msaada huo bado umesitishwa.

Wiki iliyopita kundi la Taliban limefanya mazungumzo yake ya kwanza ya ana kwa ana na wajumbe kutoka Umoja wa Ulaya na Marekani, mkutano uliofanyika huko Doha nchini Qatar.

Kundi hilo linaendeleza juhudi za kidiplomasia likilenga kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa.

Katika mkutano huo wa Qatar, Kaimu waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Taliban, Amir Khan Muttaqi aliwaomba wanaoratibu safari za Waafghanistan kwenda Ulaya kuacha mara moja ili kuboresha maisha ya watu 10 kuliko maisha ya mtu mmoja mmoja.

Msaada wa kimataifa kuelekea Afghanistan umesitishwa tangu kundi la Taliban liliporudi tena madarakani baada ya jeshi la Marekani na vikosi vingine vya kimataifa kuondoka baada ya miaka 20 ya vita katika taifa hilo.

Mali za nchi hiyo zilizoko nje zimezuiwa wakati bei ya vyakula na ukosefu wa ajira vikipanda hali ambayo inaongeza wasiwasi wa kushuhudiwa janga kubwa la kibinadamu pale msimu wa baridi kali utakapoingia.

error: Content is protected !!