January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri wa Fedha ajitosa ubunge Zanzibar

Saada Salum Mkuya

Spread the love

WAZIRI wa Fedha katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, Saada Salum Mkuya, kwa mara ya kwanza ameingia katika kinyang’anyiro cha kusaka ubunge kwa uchaguzi utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Saada, mwanamama aliyesomea masuala ya uongozi wa fedha kufikia kiwango cha shahada, amejijengea jina kubwa kiutendaji kwa kuhimili vishindo vya kushika wadhifa huo ndani ya shutuma kali za ufisadi kugubika serikali ya CCM. Alirudisha fomu ya kugombea kiti cha Welezo, nje kidogo ya mjini Zanzibar.

Welezo ni jimbo jipya la uchaguzi lililoundwa katika ugawaji mpya wa majimbo uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) mwanzoni mwa mwezi huu.

Taarifa za ndani ya Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, mjini hapa, zinasema kwamba Saada amepata washindani wawili ambao wenyewe viongozi wa chama hicho wanawaita kama “washindani wepesi mno.”

Washindani wake watakaoshiriki kura ya maoni Agosti mosi, ni Abbas Hassan Juma na Zahor Salum Mohamed. Juma ni mdogo wa mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma aliyewahi kuwa waziri katika serikali ya Amani Abeid Karume.

Saada anatafuta ubunge ikiwa ni mara yake ya kwanza. Aliitwa kwenye siasa alipoteuliwa mbunge mwishoni mwa mwaka 2013 na moja kwa moja akateuliwa naibu waziri wa fedha akiwa chini ya Dk. William Mgimwa aliyekuwa mbunge wa Ludewa.

Saada alipandishwa kuwa waziri kamili mapema mwaka 2014 baada ya Dk. Mgimwa kufariki dunia katika mazingira ya kutatanisha akiwa matibabuni nchini Afrika Kusini. Inasemekana alilishwa sumu wakati wa mgogoro uliotokea kuhusiana na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. 300 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.

Uongozi wake kama waziri umeshuhudiwa ukimpandisha chati kisiasa kwa kuwa jasiri na mahiri katika kujenga hoja za maelezo ya masuala ya mipango na utekelezaji wa bajeti ya serikali. Amefanikiwa kupitishiwa bajeti ya serikali pamoja na miswada ya inayohusu sheria mpya za kodi.

Hata hivyo, jimbo analoomba kugombea, huenda likawa na mgogoro kwa vile ni moja ya majimbo manne yaliyoongezwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na ambayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema haijayaidhinisha kutokana na kutopata muda wa kuyachunguza kama vigezo vimetimizwa.

error: Content is protected !!