January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Ummy azomewa bungeni

Waziri Ofisa ya Rais, TAMISEMI

Spread the love

MAJIBU ya uongo na upotoshaji kuhusu Muundo wa Muungano, yamesababisha Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu kuzomewa ndani ya Bunge. Anaandika Mwandishi wetu…(endelea).

Ummy amepatwa na kadhia hiyo leo asubuhi wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema).

Katika swali lake, Mnyika alisema haja ya kuwa na zamu katika nafasi ya urais kati ya Zanzibar na Tanzania Bara ni moja ya kero za Muungano kutokana na CCM kukumbatia muundo wa sasa wa serikali mbili badala ya Shirikisho la serikali tatu, uliopendekezwa na wananchi kwenye Rasimu ya Jaji Joseph Warioba ambao ungekuwa ufumbuzi  wa suala hilo.

“Lakini Katiba pendekezwa imeturudisha katika mgogoro unaoendelea, pamoja na kasoro hizi ni kwanini viongozi we serikali wameshachukua msimamo kabla ya kipindi cha kampeni ya kura ya maoni kwa kuwaambia wananchi wapige kura ya ndio kwa katiba yenye kasoro?

 “Serikali inawakataza viongozi wa dini walioanza kueleza kwamba kuna ouzo kwenye katiba pendekezwa hivyo, kuwataka watu wajiandae kupiga kura ya hapana na inawakataza Ukawa kuwaambia wananchi wasihiriki kura hiyo kwa kuwa maoni yao hayakuzingatiwa,” alihoji Mnyika. 

Swali la Mnyika lilitokana na swali la msingi la mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim Ayoub (CCM), aliyetaka kujua ni lini serikali itafanya marekebisho katika katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuweka utaratibu wa kutapa viongozi kwa awamu.

Katika majibu yake kwa Mnyika, Ummy alisema suala la muundo wa Muungano wa serikali tatu yalikuwa mapendekezo binafsi ya iliyokuwa Tume ya kurekebisha katiba chini ya Jaji Joseph Warioba na hayakuwa maoni ya Watanzania walio wengi.

Amesema kuwa maoni ya watu walio wengi, yalizungumzia elimu, afya, maji na pembejeo, kwamba ndio maana wajumbe waliobaki katika Bunge la Katiba waliona bado ipo haja ya kuendelea na serikali mbili.

“Wale waliokuwa wakitaka kuwepo na muundo wa serikali tatu kama walikuwa na hoja za mashiko wangebaki ndani na kuzungumza hoja zao,” alisema Ummy na kuongeza kuwa;

“Sio vibaya kuwaambia wananchi wapige kura ya ndiyo kwa katiba inayopendekezwa kwa kuwa kila kitu tayari kimeshaandaliwa”.

Majibu hayo yalipingwa vikali na wabunge wa kambi ya upinzani na hivyo kuanza kumcheka na kumzomea wakati wote, ingawa kwa kulazimisha aliendelea kujibu hadi pale Spika Anne Makinda alipoingia kati.

Makinda katika kusawazisha swali la Mnyika kuhusu viongozi wa dini kubanwa na serikali, amesema “wasizitumie nyumba za ibada kufanya kazi hiyo ya kushawishi waumini katika kupinga Katiba pendekezwa”.

Mapema katika kujibu swali la msingi, Ummy amesema utaratibu wa kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977 na kufafanuliwa katika sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 toleo la 2002.

 “Sifa za mtu kuchaguliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeainishwa katika ibara ya 39 ya Katiba. Serikali haina dhamira ya kufanya marekebisho ya katiba kuhusu utaratibu wa kupata viongozi wa nafasi ya urais kwa zamu kwa kuzingatia pande mbili za Muungano kwa sababu suala la uchaguzi wa Rais ni suala la kidemokrasia,” amesema.

error: Content is protected !!