October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Ummy awapiga ‘stop’ RC, DC, DED kusafiri

WaziriI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu

Spread the love

 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amewapiga marufuku wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi kutoka nje ya mkoa bila kibali cha Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Ummy ametoa maagizo hayo leo tarehe 12 Oktoba, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dodoma kwa lengo la kufafanua namna TAMISEMI itakavyotumia mkopo wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) kutekeleza miradi mbalimbali ambayo utekelezaji wake unawahusu viongozi na watendaji hao wa mikoa nchini.

Amesema wakuu wa mikoa na wakurugenzi wanatakiwa kuepuka safari zisizo za lazima za kutoka nje ya mkoa isipokuwa kwa kibali cha viongozi hao wakuu wa nchi.

Amesema hata yeye hawezi kuwaita viongozi hao bila kibali hicho, isipokuwa wakuu wa wilaya ambao wanatakiwa kupewa semina elekezi kwa muda wa siku tatu.

“Lakini kwa sababu tunajambo hili kubwa, ninawaelekeza viongozi wote wa Serikali ndani ya Tamisemi, ngazi ya mikoa, wilaya na halmashauri kuepuka safari zisizo za lazima zinazohusu kutoka nje ya mkoa wako isipokuwa kwa kibali cha viongozi wakuu wa nchi.”

“Kwa hiyo mkuu wa mkoa ukitaka kutoka ndani ya Mkoa wako kipindi hiki lazima upate kibali cha rais, kibali cha Makamu wa Rais au Waziri Mkuu.

“Tunataka wabaki katika mikoa yao,  tunataka wasimamie utekelezaji wa miradi hii hata mimi waziri wa Tamisemi kama nitawaita maana yake lazima nipate kibali cha rais au waziri mkuu, makamu wa rais cha kusema waziri nimekuruhusu uwaite wakuu wa mikoa, wakurugenzi watoke ndani ya halmashauri zao,” amesema Ummy.

Aidha, amesema katika mkopo huo nafuu wenye thamani Sh trilioni 1.3 uliotolewa kwa Tanzania, Mamlaka ya Serikali za Mitaa imeidhinishiwa kiasi cha Sh bilioni 535.68 kutekeleza miradi mbalimbali

“TAMISEMI imeidhinishiwa Sh bilioni 535.68 kati ya fedha zote zilizotolewa kwenye mkopo huo wa masharti nafuu ambayo ni sawa na asilimi 41.1 kati ya fedha hizo Sh bilioni 304 ni kwa ajili ya elimu msingi, Sh bilioni 226.68 ni kwa ajili ya afya ya msingi na Sh bilioni 5.00 ni kwa ajili ya kuboresha miundombinu.

“Matumizi ya fedha hizi zimeelekezwa kwenye maeneo ya vipaumbele vinavyogusa wananchi moja kwa moja kwa ajili ya kuwaondolea kero katika kuzifikia na kuzipata huduma za afya, elimu na uwezeshaji wananchi kiuchumi, vilevile kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.

“Mathalani Serikali imepanga kujenga vyumba vya madarasa 12,000 vitakavyogharimu Sh bilioni 240 katika shule za sekondari katika Halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kujiandaa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza watakaojiunga mwezi Januari, 2022″ amesema.

Aidha, amewaelekeza wakuu wa Mikoa na Wilaya Kuunda Kamati ya Mkoa ya uratibu na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi husika na kuhakikisha kwamba zinawasilisha kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI taarifa ya utekelezaji wa miradi kila baada ya wiki mbili.

“Naelekeza Kuhakikisha utekelezaji wa miradi unaanza ndani ya wiki mbili mara baada ya fedha kupokelewa; miradi ya madarasa ikamilike kabla au ifikapo tarehe 15 Desemba 2021 na miradi mingine ikamilike kabla au ifakapo tarehe 30/04/2022”

“Naelekeza utekelezaji wa miradi hiyo uzingatie Thamani ya fedha na ubora wa miradi pia watoa huduma wa vifaa, mafundi watangaziwe kazi  zilizopo kupitia tovuti za Mikoa, Halmas hauri pamoja na mbao za matangazo katika ofisi za umma” amesema.

Aidha, amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kuwa na Kamati ya Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi kwa ajili ya kuratibu utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha fedha zinakwenda haraka.

error: Content is protected !!