August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Ummy atoa tahadhari ya Uviko-19: Kumekuwa na ongezeko la mafua

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Spread the love

 

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu, amewataka wananchi wachukue tahadhari za kujikinga dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19), kwani bado upo na kwamba maambukizi yake ni asilimia tano. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ummy ametoa tahadhari hiyo leo Jumanne, tarehe 26 Julai 2022, alipokuwa anapokea vifaa vya kupimia UVIKO-19 na hewa ya Oksijeni, kutoka kwa Serikali ya Australia, kwenye ofisi za Bohari Kuu ya Dawa (MSD), jijini Dar es Salaam.

Waziri huyo wa afya amesema, wiki hii kumekuwa na ongezeko la ugonjwa wa mafua na pia watu 160 kati ya 2,708 waliopima ugonjwa huo, wamekutwa na maambukizi ya UVIKO-19.

“Nisisitize ugonjwa wa UVIKO-19 bado upo , kama mnafuatilia wiki hii kuna watu vifua na mafua yamezidi. Hata jana kuna rafiki yangu wa karibu ameniambia wamelala wameamka dada yake amefariki na alikuwa na tatizo la upumuaji. Kwa hiyo bado ugonjwa wa UVIKO-19 upo,” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amewataka wananchi wachome chanjo ya UVIKO-19 ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Kuhusu vifaa tiba alivyovipokea, Ummy amesema amepokea katoni 2,000 vya vipimo vya haraka vya UVIKO-19 vitakavyopima watu zaidi ya 20,000. Pamoja na vifaa vya kupima hewa ya oksijeni mwilini 1,000 ambavyo vitasambazwa katika vituo vya kutoa huduma ya afya 500 hususan zahanati.

error: Content is protected !!