Friday , 3 February 2023
Home Kitengo Maisha Afya Waziri Ummy achambua takwimu za saratani
Afya

Waziri Ummy achambua takwimu za saratani

Spread the love

 

WAZIRI wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema, katika kila watu 100,000 watu 76 hugundulika kuwa na ugonjwa wa Saratani. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Ummy amesema hayo leo Ijumaa, tarehe 4 Februari 2022 jijini Dodoma, wakati akitoa tamko la siku ya saratani duniani.

Amesema sababu nyingine inayochangia saratani ni unene uliokithiri, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, matumizi ya pombe kupita kiasi na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda, matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi.

Waziri Ummy amesema kutokana na changamoto hiyo, Serikali imeimarisha huduma za kibingwa katika hospitali sita za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi na tiba kwa kuongeza wataalam, miundombinu pamoja na vifaa tiba.

Amesema takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2018, zikionesha kuwepo kwa wagonjwa wapya 42,060 kwa mwaka na takribani wagonjwa 28,610 sawa na asilimia 68 hufariki kutokana na ugonjwa huo.

Katika taarifa za mwaka 2021 kutoka kanzi data ya wagonjwa iliopo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonesha Saratani zinazoathiri wanaume zaidi ni pamoja na saratani ya tezi dume (21%), Saratani ya Koo (11.8%) na Saratani ya utumbo mkubwa na mdogo (9%).

Zingine ni Saratani ya mdomo na kinywa (7.3%) na kwa upande wa wanawake saratani zinazowaathiri zaidi ni pamoja na Saratani ya Mlango ya Kizazi (43%), Saratani ya Matiti (14.2%) na Saratani ya koo (3.8%).

Waziri Ummy ameweka wazi saratani ni ugonjwa ambao unaathiri watu wa rika na jinsia zote watoto, watu wazima, wanawake na wanaume ambapo takwimu za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO), 2018 zinaeleza kila mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1, na kati ya hao, zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki kutokana na ugonjwa wa saratani kila mwaka ambao ni sawa na takribani asilimia 50.

Aidha, zaidi ya watu ya millioni 43.8 wanaishi na saratani duniani.

“Kama hatua madhubuti za kinga, uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la saratani linakadiriwa kuongezeka na idadi ya wagonjwa wapya kufikia milioni 24 ifikapo mwaka 2035, huku ongezeko kubwa likiwa katika ukanda wa nchi zinazoendelea kama Tanzania”.

Vile vile amesema takwimu kutoka kwenye kanzi data zilizo anzishwa kwa Kanda, zinaonesha wagonjwa wapya 14,136 walifikiwa na huduma ambayo ni sawa na asilimia 33 ya makadirio ya wagonjwa wapya wote kwa mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia tano ukilinganisha na takwimu za Mwaka 2020 ambapo jumla ya wagonjwa wapya 12,096 (28%) walionwa.

“Ongezeko la wagonjwa wa saratani pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza, linachangiwa zaidi na mtindo wa maisha usiozingatia afya bora kama kutokufanya mazoezi (Tabia Bwete), unene uliokithiri, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, matumizi ya pombe kupita kiasi na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda, matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi”, amesema Waziri Ummy.

Waziri huyo amesema, kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani zinazochangiwa na mtindo wa maisha ikilinganishwa na ilivyokuwa awali ambapo wagonjwa wengi walikuwa ni wale wenye saratani zinazotokana na maambukizi ya virusi.

“Ni vyema kila mmoja akapima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya kiafya. Endapo utatambuliwa kuwa una ugonjwa wa Saratani tumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya,” amesema

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Afya

Ma-RMO, DMO watakiwa kujitafakari ubadhirifu hospitali za mikoa, wilaya

Spread the love  NAIBU Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, amewataka waganga...

Afya

JK atoa ya moyoni kuhusu huduma za afya

Spread the love  RAIS Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete amesema huduma za afya...

AfyaHabari za Siasa

Heche amvaa Ummy Mwalimu kisa bima ya afya

Spread the love  MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche amemtaka...

Afya

Asilimia 86 wenye umri zaidi ya miaka 18 wapata dozi kamili ya Uviko-19

Spread the love  KWA kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi Julai hadi...

error: Content is protected !!