January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Simbachawene: Hakuna umuhimu wa katiba mpya

George Simbachawene, Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania

Spread the love

 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, George Simbachawene amesema, kwa sasa hakuna umuhimu wa Katiba mpya kwani iliyopo inajitosheleza na imeivusha nchi hiyo kwenye kipindi kigumu. Anaripoti Glory Massamu, TUDARCo … (endelea).

Simbachawene amesema uimara wa Katiba ya sasa ya Tanzania umeleta amani, kupendana, kushirikiana na kuwepo kwa kasi ya maendeleo nchini.

Ameyasema hayo leo Jumatano, tarehe 22 Septemba 2021, Kijiji cha Makose na Chogola, Kata ya Masa, jimboni kwake Kibakwe, wilayani Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma.

“Tanzania hakuna tatizo la Katiba maana hii iliyopo ni nzuri na imetupitisha katika vipindi muhimu na vigumu,” amesema Simbachawene

Amesema vyama vya upinzani wanaitaka Katiba mpya si kwa ajili ya wananchi bali kwa malengo yao binafsi hivyo hakuna umuhimu wa kuwepo kwa mchakato wa Katiba mpya.

Simbachawene amesema, hakatai Katiba inaweza kuwa na upungufu kwa baadhi ya vipengele, hivyo vyama vya upinzani wanapaswa kueleza eneo lipi lifanyiwe mabadiliko kama lipo na siyo kutaka katiba nzima ibadilishwe wakati bado ina ubora wa hali ya juu na ndiyo imeleta maendeleo makubwa nchini.

Taarifa iliyotumwa kwa umma na ofisi ya wizara hiyo imesema, sekeseke na vurugu nyingi za vyama vya upinzani ni kuzungumzia katiba ambayo haina kosa lolote na shida kuu ya wananchi ni vitu vya maendeleo na siyo Katiba.

“Unakuta mtu anaisema Katiba mbaya kwa kipengele kimoja tu cha tume ya uchaguzi, baasi, lakini Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo iliyotuweka katika hali ya kupendana na nchi ya Amani.

“Katiba hii ya Tanzania ndio inayopelekea Watanzania wanamiliki rasilimali na maliasili kwa umoja bila kuwa na ugomvi,” amesema Simbachawene.

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) na Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein (katikati) wakionesha katiba Mpya

Akiendelea kuzungumza, Simbachawene amesema “Katiba ya Tanzania ni nzuri na hakuna kitu ambacho hakikosi mapungufu, hivyo mapungufu ya hapa na pale yanaweza yakawa yapo na yanapaswa kushughulikiwa na siyo kwa kuibomoa Katiba yote.”

Wakati Simbachawene akizungumzia suala la Katiba mpya, yeye mwenyewe alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambalo lilijadili Rasimu ya Katiba na kupatikana kwa Katiba pendekezwa ikisubiri kura ya maoni.

Aidha, Simbachawene aliwataka wananchi wa Kata Masa kuhakikisha wanatunza mazingira kwa kutokata miti, kuharibu vyanzo vya maji na kusababisha barabara, mashamba, madaraja kuharibika kutokana na maporomoko ya maji kutoka milimani baada ya baadhi ya wananchi kuharibu mazingira hayo.

“Afisa mtendaji wa Kata nakuagiza hakikisha unalinda misitu, wachukulie hatua kali wanaokata miti, wanaolima milimani.

“Nipo tayari nikose kura zao kwa wale ambao wanasababisha uharibifu wa mazingira, jamani kutunza mazingira ni muhimu, lazima mlijue hili, msifanye mzaha,” amesema Simbachawene

Simbachawene amemaliza ziara jimboni kwake kwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

error: Content is protected !!