July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Possi: Ajirini walemavu

Spread the love

DAKTARI Abdallah Possi, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye ulemavu) amevitaka vyombo vya habari nchini kuandaa sera endelevu ya kuajiri walemavu na kutumia lugha za alama ili kuleta usawa katika soko la ajira na upashaji wa habari, anaandika Regina Mkonde.

Amesema hayo kwenye kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam leo wakati akizungumza na wamiliki wa vyombo vya habari nchini.

“Vyombo vya habari inabidi vianzishe mpango na sera endelevu ya kuajiri watu wenye ulemavu ili kuleta usawa katika soko la ajira kama sheria ya 9 ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 inavyosema,” amesema Dk. Possi.
Possi amekumbusha vyombo hivyo juu ya mkataba wao na TCRA wa kutoa habari kwa lugha za alama ili kuwezesha watu wenye ulemavu wa kusikia kupata fursa ya kuhabarika.
“Vyombo vya habari vina wajibu wa kutumia lugha za alama wakati wa utoaji habari kama TCRA inavyotaka, hivi karibuni nitatoa tangazo katika gazeti la serikali la kuvitaka vyombo vya habari kutumia lugha za alama,” amesema.
Pia, vyombo vya habari vimetakiwa kuanzisha dawati la habari za walemavu ili kueleza changamoto zao, mafanikio yao na kwamba itasaidia kutobaguliwa na kuonekana kama watu wengine.
“Imezoeleka kwa vyombo vya habari kutoa habari za udhaifu, na changamoto zao jambo linalochochea walemavu kudharaulika na kuonekana dhaifu katika shughuli za maendeleo nchini,” amesema.
Hivi karibuni TCRA iliandikia barua kwa vyombo vya habari hasa Runinga kuvitaka kutumia lugha za alama kuanzia tarehe 15 Machi mwaka huu.
“TCRA hivi karibuni imetoa muda kwa Runinga zote nchini kuanza kutumia lugha za alama ifikapo 15 Machi 2016, kwa atakaye kaidi hilo, atapata adhabu kutoka kwa TCRA na kutoka kwangu baada ya kutoa tangazo langu,” amesema.

error: Content is protected !!