December 4, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Ndaki ataka ufugaji wenye tija kwa makundi ya wafugaji

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akikabidhi madume ya ng'ombe kwa wafugaji wa Maswa

Spread the love

 

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, ameyataka makundi ya wafugaji nchini kufanya ufugaji wenye tija kwa kutumia ng’ombe aina ya borani ili kujiongezea pato na kumiliki uchumi. Anaripoti Paul Kayanda, Simiyu … (endelea).

Amesema kuwa kwa sasa serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuja na mageuzi kwa kufuga mifugo bora na yenye tija kupitia ng’ombe aina ya borani ili kupata kilo nyingi, nyama nyingi na kuzalisha maziwa mengi jambo ambalo litachangia pato la taifa.

Waziri Mashimba aliyasema hayo jana wakati akikabidhi madume 50 ya ng’ombe aina ya borani kwa makundi ya wafugaji wa wilaya ya maswa kwenye hafla fupi iliyofanyika kwenye Kata ya Buchambi mkoani hapa.

“Kiasi cha Sh 915 milioni kilichotolewa na serikali kimetumika kununua madume 336 ya ng’ombe aina ya borani ambayo yatakabidhiwa kwenye wilaya 10 nchi nzima, hapa Wilaya ya Maswa tumekabidhi haya madume 50, ombi langu muwatunze kwa kuwaosha mara kwa mara ili wasipate kupe wakapata ugonjwa wa ndigana,” alisema Waziri Mashimba.

Waziri Mashimba aliongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ng’ombe hao bure kwa vikundi vyote vya wafugaji na kila kikundi kitapata dume moja ambalo litapanda majike yasiyopungua 25 kwa mwaka lengo ni kuzalisha ng’ombe wa kisasa na bora zaidi kwa ufugaji.

Alisema kuwa mpango wa serikali ni kuhamasisha ufugaji wa kisasa wa mifugo michache na kipato kingi na kuongeza kuwa aina hiyo ya Ng’ombe ni tofauti na ng’ombe wa kawaida na kufafanua kuwa ngo’ombe wa kienyeji wanne ni sawa na ng’ombe mmoja aina ya borani.

“Niwaambieni tu kuwa kwa madume haya ng’ombe atakayezaliwa ana uwezo wa kutoa lita 5 mpaka 10 kwa siku lakini wa kienyeji akijitahidi sana anaweza kutoa lita 1 mpaka 5 kwa siku kwa hiyo ngombe wa kienyeji anaingizia serikali pato dogo,” alisema Waziri Mashimba.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa Aswege Kaminyonge amebainisha changamoto kubwa ni ukosefu wa pikipiki zitakazotumika katika mizunguko kwenye vijiji mbalimbali ili kufuatilia mradi huo usije ukakwama.

Vile vile mkuu huyo wa Wilaya aliwataka maafisa watendaji wa Kata kufuatilia kwa ukaribu zaidi wafugaji wote waliokabidhiwa madume hayo ili yasidhulike kwa kukosa matunzo.

Kwa upande wake Jossan Ntangeki mmiliki wa shamba la Mifugo Mkoani Kagera ambaye ameambatana na Waziri huyo alisema kuwa Madume hayo kati ya mwaka mmoja hadi miwili na yamepatiwa huduma zote za chanjo na kuwaomba wafugaji kujitahidi kuwapatia huduma za chanjo kwa wakati huku akiwataka wengine wenye nia ya kufanya ufugaji wa kisasa wafike kwenye shamba lake.

error: Content is protected !!