May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Mwambe asema corona imepandisha bei ya mafuta ya kula

Spread the love

WAZIRI wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Geofrey Mwambe amesema, kupanda kwa bei ya mafuta ya kula, kumesababishwa na mfumuko wa bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia, uliosababishwa na athari za mlipuko wa virusi vya corona (COVID-19). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mwambe amesema hayo leo Jumanne tarehe 12 Januari 2021, wakati anatoa ufafanuzi wa sakata la kupanda kwa bei ya mafuta ya kula nchini.

Amesema bei ya mafuta katika soko la dunia ilianza kupanda Julai 2020 na kwamba Oktoba 2020 bei ya mafuta ilikuwa Dola za Marekani 786 kwa metric tani 1, hadi kufikia Januari 2021 bei hiyo ilizidi kupanda hadi Dola 1,075, kwa ujazo huo.

“Kuanzia mwezi wa saba mwaka jana, bei zimeanza kupanda kwenye soko la dunia, mfano mwezi wa kumi bei ilifika Dola 786 kwa metric tani moja mpaka inafika hapa. Lakini kwa mwezi wa kwanza 2021 imefika dola 1,075, kwa hiyo unaweza kuona hilo ongezeko,” amesema Mwambe.

Kwa mujibu wa baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta nchini, mafuta ya kula yanayotoka nje ya nchi, yamepanda bei kutoka Sh.50,000 kwa lita 20 hadi kufikia Sh.90,000 katika baadhi ya maeneo.

Mwambe amesema, ongezeko hilo la bei limechangia kupanda kwa bei ya mafuta nchini, kwa kuwa asilimia kubwa mafuta yanayotumiwa nchini, yanatoka nje ya nchi.

Waziri huyo amesema, mlipuko wa corona umechangia kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo, kwa kuwa umesababisha kusuasua kwa uzalishaji na usafirishaji wa mafuta ya kula duniani.

“Kwa kuwa nchi zinazozalisha bidhaa hiyo zimeweka watu wake karantini, kwa ajili ya kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa kali inayosababishwa na virusi hivyo(Covid-19), ikiwemo kudhibiti maambukizi yake,” amesema.

Mlipupuko wa Virusi vya corona ulianzia nchini China mwishoni mwa mwaka 2019, kisha ukasambaa duniani kote.

Geofrey Mwambe, Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania

“Hilo ongezeko limetokana na sababu nyingi lakini kubwa, corona ina athari kubwa sana, sisi kwetu tuna mshukuru Mungu hatuna corona, wenzetu athari za corona ni kubwa,” amesema Mwambe ambaye pia ni Mbunge wa Masasi (CCM), Mkoa wa Mtwara.

Mwambe amesema “kwanza kwenye ulimaji, sababu haya mafuta kwa kiasi kikubwa tunachukua mafuta ya mawese ambao wenzetu huwa wanatengeneza. Na sisi kwa kiasi kikubwa tunachukua nchini Malasia.”

“Kwa hiyo, kuna suala la uzalishaji kwanza, wakati watu wanakimbizana kule na corona na kujifungia ndani uzalishaji unapungua. Lakini pili kwenye kuchakatwa, viwanda vile vya kusafisha havifanyi kazi kama kawaida, wanachukua watu wachache ili kuchukua tahadhari ya corona.”

Sambamba na kupungua kwa uzalishaji wa mafuta, Mwambe amesema, usafirishaji wa bidhaa hiyo kuingia nchini umekuwa wa kusuasua kutokana na athari za virusi vya corona.

“Lakini pia upande wa usafirishaji umekuwa shida, kufanya mipangilio kupata meli nayo ni shida. Sababu hata makampuni ya meli nayo wanahangaika na corona, wengine wanafariki, wanaumwa na ofisi zinafungwa,” amesema Mwambe.

Hata hivyo, Mwambe amewatoa wasiwasi Watanzania akisema kwamba, mafuta ya kula yaliyoingizwa nchini tarehe 5 Januari 2021, yatapakuliwa bandarini tarehe 19 Januari 2021.

“Lakini bahati nzuri, pia tuna meli mbili ambazo zimeshafika, moja imefika tarehe 10 Desemba 2020 na imeshamwaga mafuta yake pale lita 21,800 na nyingine imefika tarehe 5 mwezi huu. Kwa hiyo imepangiwa kupakua tarehe 19 mwezi huu,” amesema Mwambe.

Amesema Serikali itasimamia usambazwaji wake ili kuhakikisha yanawafikia Watanzania wote.

“Ingawa tunawasiliana na waziri mwenzangu wa uchukuzi na mawasiliano ili ikiwezekana ipangiwe kushusha mapema zaidi, kama stoo zao zina nafasi ili tuhakikishe mafuta yanapatikana.

Tunaendelea kuyaingiza kwenye soko kwa uhakika, kuhakikisha mafuta yanapatikana kama ilivyopangwa,” amesema Mwambe.

Mwambe amesema Serikali inaendelea kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi ili kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa wakati.

“Na bahati nzuri ile meli itakayoshusha mafuta hivi karibuni, waagizaji wake nimeongea nao na meli nyingine zitakuja siku 45 zijazo. Kwa hiyo, tayari mafuta mengine yako katika utaratibu wa kuja. Kwa hiyo Februari mafuta yanaingia tena,” amesema Mwambe.

Ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafuta ya kula na kupanda kwa bei yake, Mwambe amesema Serikali itahakikisha inaingiza mafuta kila mwezi.

“Tutahakikisha kila mwezi yanaingia, sababu kwa mwezi tunatumia metric tani 30,000 kama nchi, tunayoagiza kutoka nje. Achilia mbali tunayozalisha ndani , kwa hiyo tutahakikisha kwamba mafuta yanakuja kila wakati, hatukwami,” ameahidi Mwambe.

Pamoja na hilo, Mwambe amesema Serikali itatoa upendeleo kwa meli zinazoingiza mafuta ya kula nchini, ikiwemo kuziwekea utaratibu mzuri wa kuingia pamoja na kupakua mzigo wake.

“Lakini la pili kutoa upendeleo kwa meli zinapokuja za mafuta ya kula, ili mafuta yasiadimike kwa sababu tu meli imechelewa kutia nanga. Sababu ile ghati tunayotumia, tunatumia kwa mafuta mengine kwa hiyo tutahakikisha kwamba tunatengeza ratiba nzuri ya mafuta yaweze kupakuliwa mapema,” amesema Mwambe.

Mwambe amesema, Serikali itatoa mashamba kwa wawekezaji watakaokuwa tayari kulima michikichiki, karanga na alizeti, ili kupata malighafi za kutosha za kutengeneza mafuta ya kula yatakayokidhi mahitaji ya Watanzania.

“La tatu ambalo ni kubwa, nimeongea na hao wazalishaji nimewaambia sisi wenyewe tuna uwezekano mkubwa wa kuzalisha wenyewe mafuta hapa ndani. Bahati nzuri nimefanya mazungumzo nao wamekubali wataandika barua rasmi ya kuomba niwapatie mashamba,” amesema Mwambe.

error: Content is protected !!