Tuesday , 30 May 2023
Home Kitengo Michezo Waziri Mwakyembe asiturudishe nyuma
MichezoTangulizi

Waziri Mwakyembe asiturudishe nyuma

Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Spread the love

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ametangaza rasmi, kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni kutumika katika mchezo mmoja. Anaandika Yusuf Aboud … (endelea).

Agizo hilo la Waziri Mwakyembe linaanza kutekelezwa Msimu huu wa Ligi (2019/20), ambapo ni wachezaji watano tu wa kigeni ndiyo watakaoruhusiwa kutumika katika mchezo mmoja, badala ya wote 10 wanaoruhusiwa kusajiliwa.

Dk. Mwakyembe anadai kufanya hivyo kutalinda ajira za Watanzania, lakini pia kutasaidia kukuza soka letu.

Kwangu mimi naona Pepo la kudumaza soka letu bado linawaandama viongozi wetu wenye mamlaka ya kuamua hatma yetu.

Kwanza; Dk. Mwakyembe anazungumzia kuhusu kulinda ajira za Watanzania. Kwa mtazamo wake watakaporuhusiwa wachezaji watano badala ya 10 kucheza katika mchezo mmoja, ndiyo itasaidia kulinda ajira za wachezaji watano wa ndani.

Nimkumbushe Mwakyembe, kwamba ajira haipo katika kucheza mchezo mmoja ndani ya kiwanja, bali ni katika kusajiliwa. Ukimsajili mtu (kumuajiri) hata kama hukumtumia lakini utalazimika kumlipa, na hiyo ndio ajira.

Kama unaruhusu waajiriwe wachezaji 10 wa kigeni, huwezi kulinda ajira za wachezaji wa ndani eti kwa kuzuia watano wasicheze katika mchezo mmoja.

Timu zinasajili wachezaji 30, miongoni mwao wanaruhusa ya kusajili 10 kutoka mataifa mengine, maana yake idadi ya Watanzania anaowalinda Mwakyembe itakuwa 20, hata ukiwazuia wasicheze wote 10 katika mchezo mmoja, bado Watanzania watakaopata ajira ni walewale 20.

Kama lengo ni kulinda ajira za wazawa, basi angetoa amri ya kusajili wachezaji watano, ili hizo nafasi tano nyingine wazipate Watanzania.

Pili; Dk. Mwakyembe anaamini tukipunguza idadi ya wachezaji wa kigeni soka letu litakua zaidi na hata timu ya taifa itakuwa imara kuliko ilivyo sasa.

Sijui kama Mwakyembe alijishughulisha kufanya utafiti japo mdogo, au labda alihofia sheria ya Takwimu, maana ukifanya utafiti utapaswa kutoa takwimu zako.

Ipo hivi; kupunguza au kuondoa wachezaji wa kigeni katika Ligi yetu hakutasaidia kukuza soka letu, bali kutaturudisha hatua 10 nyuma.

Uwepo wa wachezaji wa kigeni wenye viwango kwenye Ligi zetu, unasaidia kuimarisha wachezaji wetu wa ndani na kuongeza ubora wa Ligi zetu.

Twende kwa mifano;

Mosi; Katika msimu wa 2018/19, timu ya Simba ya Tanzania ilifika hatua ya Robo fainali ya michuano mikubwa zaidi kwa klabu Afrika.

Sababu kuu Simba ilisajili kikosi bora cha kushindana na klabu za mataifa mengine. Kwa wakati mmoja Simba ilitumia wachezaji wanane wa kigeni katika mchezo mmoja ili kuipa ushindi timu hiyo.

Iliwatumia Zana Coulibaly, Juuko Murshid, Pascal Wawa, James Kotei, Cloutus Chama, Haruna Niyonzima, Medie Kagere na Emmanuel Okwi.

Wachezaji hawa kwanza walicheza pamoja kwenye michezo ya Ligi ya ndani ili kuzoeana na ndipo walipokuja kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Huwezi kusajili wachezaji 10, kwenye Ligi ukawatumia watano, lakini kwenye michuano ya kimataifa ukawatumia wote 10 kwa wakati mmoja. Ni lazima kwanza wacheze michezo mingi ya Ligi pamoja, ili kuzoeana na kutengeneza timu imara.

Kwa kutumia wachezaji wa kimataifa, Simba ilipata ushindi ulioleta sifa kwa taifa. Ushindi wa Simba kimataifa uliongeza thamani ya Ligi yetu, lakini pia ushiriki na ushindi wa Simba uliingizia taifa fedha za kigeni.

Pili; Ligi zetu haziwezi kuimarika na kuwa bora kwa kutumia wachezaji wazawa wenyewe, huku ni kujidanganya. Waziri Mwakyembe aelezwe ukweli aelewe.

Na wala hatuwezi kupata timu ya taifa lilio imara kwa kutumia wachezaji wanaocheza katika Ligi zetu za ndani.

Kwa kuwa Taifa halina wachezaji wengi wanaocheza katika Ligi kubwa za nje, ambao wangekuja kuunda timu bora ya taifa, sio vibaya Ligi yetu kukaribisha wageni, angalau wachezaji wetu wataongeza kitu katika taaluma yao.

Tatu; Waziri Mwakyembe na wote wenye mawazo kama yake waelewe kwamba, wageni waliopo kwenye Ligi yetu wamesaidia sana kuwaongezea ubora wachezaji wetu wa ndani na kuifanya timu yetu ya taifa kuimarika kiasi.

Kwa mfano, Taifa Stars ilipocheza na Uganda, wachezaji wetu kina Erasto Nyoni, Aishi Manula, Kelvin Yondani, Agrey Moris na wengine hawakupata taabu sana sababu Emmanuel Okwi na Juuko Murshidi wa Uganda wanapambana nao mazoezini na kwenye mechi za Ligi.

Simba inapofanya mazoezi, kipa wa Stars Aishi Manula anapamba na michomo ya kina Okwi wa Uganda, Chama wa Zambia, Kagere na Niyonzima wa Rwanda, timu zetu za taifa zitakapokutana, Manula hatakuwa na ugeni na washambuliaji hao, lakini pia atakuwa ameimarika zaidi kuliko mazoezini angekutana na John Bocco na Adam Salamba peke yao

Nne; Katika michuano ya AFCON inayoendelea nchini Misri, wageni wanaocheza soka Tanzania wamesaidia sana kuitangaza Ligi yetu.

Emmanuel Okwi wa Simba na timu ya taifa ya Uganda, Thaban Kamusoko wa Yanga na Zimbabwe, Jonathan Nahimana wa KMC na Burundi wameonyesha viwango vizuri, hapana shaka wapenda soka na mawakala watafuatilia Ligi wanazocheza.

Hii ni faida kubwa kwa Ligi yetu na wachezaji wetu kutupiwa macho na mawakala na wasaka vipaji, huwezi kuipata faida hii kama utaleta mawazo ya uzawa!

Kinachotakiwa wachezaji wetu wajitambue, wajitume, wapambane kugombea namba, lakini pia watafute timu nje ya nchi ili kuwaongezea maarifa wapate kulisaidia taifa lao.

Kuwazuia wageni katika Ligi zetu ni kuogopa ushindani, hakutaongeza ajira kwa wazawa, wala hakutawaongezea maarifa wachezaji wetu na matokeo yake tutadidimiza zaidia soka letu.

Kama Mwakyembe anataka kuwa na timu bora ya taifa, anachotakiwa ni kuwa na Ligi Bora ambayo itatoa wachezaji imara ambao wataweza kuleta ushindani na kupata soko kwa timu za nje.

Ukiangalia timu zinazoshiriki Fainali ya AFCON nyingi zina wachezaji wanaocheza nje, mfano Senegal inajengwa na wachezaji wote wanaocheza nje, kupata wachezji wengi wanaocheza nje siyo kuwazuia wageni bali kuwa na Ligi Bora ambayo inawapa uwezo wachezaji wazawa.

Timu za Afrika Kaskazini zimeundwa na wachezaji wageni na wa ndani, lakini wandani wameweza kuzisaidia timu zao kwani wanatokea katika timu zinazoshiriki Ligi bora Afrika.

Mwakyembe anachotakiwa kufanya ni kuboresha ligi ya ndani na kuanzia mfumo mzuri wa kukuza vipaji vya wachezaji ambao siku za usoni watakuwa bora kuliko kina Okwi, Chama, Kamusoko na wengine.

Mwakyembe asifuate njia za Joseph Mungai, Waziri wa Elimu aliyefuta michezo mashuleni na kusababiaha maafa katika sekta ya michezo nchini.

Pepo la kudumaza soka letu limuondoke Waziri Mwakyembe.

0784 44 70 77.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Uamuzi juu ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi 13 Juni

Spread the love  MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACHPR), imepanga...

Habari MchanganyikoTangulizi

Jeshi la Polisi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika utafiti

Spread the love  JESHI la Polisi Nchini limesema kuwa katika kukabiliana na...

KimataifaTangulizi

Mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda akamatwa Afrika Kusini

Spread the love  MMOJA wa watuhumiwa wakuu wa mauaji ya Kimbari ya...

Michezo

NBC Dodoma Marathon yazinduliwa, wakiambiaji 6,000 kushiriki

Spread the loveBENKI ya NBC imetangaza kufanyika kwa mbio kubwa za NBC...

error: Content is protected !!