Friday , 19 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Waziri Mkuu Majaliwa afungua maonyesho ya Sabasaba, tozo 163 zafutwa 
Habari Mchanganyiko

Waziri Mkuu Majaliwa afungua maonyesho ya Sabasaba, tozo 163 zafutwa 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kufungua Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Nne ya Dar es Salaam
Spread the love

WAZIRI MKuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuviwezesha viwanda vidogo sana, vidogo na vya kati kukua na kufanya kazi kwa tija zaidi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ametoa kauli hiyo jana jioni Ijumaa, tarehe 3 Julai , 2020 wakati akifungua rasmi Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (44TH DITF) yaliyoanza Julai mosi, 2020 kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu, Majaliwa alifungua maonesho hayo kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli.

Majaliwa alisema ili nchi iweze kuwa na mafanikio makubwa, taasisi za kifedha hazina budi kuweka mikakati ya kutoa huduma ya mikopo rafiki ili kuwezesha ukuaji wa viwanda kwa kuzingatia viwanda vidogo na vya kati ikiwemo vinavyoratibiwa na SIDO katika kila mkoa.

“Taswira hii ya maendeleo ya sekta ya viwanda inafanana na taswira ya maendeleo ya viwanda katika nchi karibu zote duniani.”

“Kwa mfano, Japan, viwanda vidogo sana, vidogo na vya kati vinachukua takribani asilimia 99 ya sekta ya viwanda; Kenya asilimia 98; Malaysia asilimia 97.3; Indonesia asilimia 99.9; Canada asilimia 98 na Ujerumani asilimia 99,” alisema.

Alisema Serikali inaendelea kuimarisha sekta ya biashara na viwanda nchini ili kuchochea maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Akielezea mafanikio ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano, Waziri Mkuu amesema, “jumla ya viwanda vipya 8,477 vimejengwa na kuchangia kuzalisha ajira mpya 482,601… mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa kwa mwaka 2019 ulikua kwa asilimia 8.5 ikilinganishwa na asilimia 8.05 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 0.45.”

Alisema mchango huo, ni matokeo ya kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji wa bidhaa viwandani nchini ambao unaendelea kuimarika na kukua vizuri.

Akitoa mfano, waziri mkuu alisema, mwaka 2019, bidhaa za viwanda zilikuwa na thamani ya Sh. 10.2 trilioni ikilinganishwa na Sh. 9.6 trilioni mwaka 2018 ambao ukuaji wake ni sawa na asilimia 5.8.

Kuhusu viwanda vidogo na biashara ndogo, waziri mkuu amesema sekta hiyo inaendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa wa wastani wa asilimia 35 kwa mwaka.

“Kwa mwaka 2019/2020, jumla ya miradi 304 inayohusiana na ujenzi wa viwanda imesajiliwa ambayo inatarajiwa kuongeza jumla ya ajira 11,793.”

Alisema SIDO imeratibu na kuhudumia viwanda vidogo vipya 1,400 vinavyotoa ajira 4,200.

“Sekta hii muhimu imeajiri Watanzania zaidi ya milioni tisa ikiwa ni ya pili kwa sekta za kiuchumi katika kutoa ajira baada ya sekta ya kilimo,” alisema.

Alisema maendeleo ya uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini yameongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo bidhaa za chuma, saruji, vigae, nguo na mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi, kusindika nyama, chakula, mbogamboga na matunda, maziwa, mafuta ya kula, sukari, vifungashio, mbolea, dawa za binadamu, sabuni na sigara pamoja na ubanguaji wa korosho.

Kwa upande wa biashara, Majaliwa alisema, utekelezaji wa Blueprint for Regulatory Reform to Improve Business Environment umewezesha maboresho ya tozo 173 ambapo kati ya tozo hizo, tozo 163 zimefutwa na tozo kero 10 zimepunguzwa viwango.

“Kati ya tozo zilizofutwa, 114 ni za sekta ya kilimo na mifugo, tano ni za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), 44 za Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka za Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), utalii, maji, uvuvi na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).”

Alisema tozo zilizopunguzwa za GCLA, zimewezesha kuhamisha jukumu la usimamizi wa masuala ya chakula kutoka iliyokuwa TFDA kwenda TBS ili kuondoa muingiliano wa majukumu. “Maboresho hayo yamesaidia kuondoa urasimu na kupunguza gharama za kufanya biashara,” alisisitiza.

Mapema, akimkaribisha Majaliwali kuzungumza na washiriki wa maonesho hayo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema, kati ya mwaka 2015 na 2019, viwanda 8,477 vilianzishwa katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kati ya hivyo, viwanda 201 ni vikubwa, 460 ni vya kati, 3,406 ni vidogo na 4,410 ni vidogo sana.

“Uwepo wa viwanda vyetu vya ndani, ulitusaidia hata wakati wa janga la corona tuliweza kutengeneza barakoa, mavazi ya watoa huduma, vitakasa mikono na bidhaa nyingine nyingi.”

Akisisitiza matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini, Waziri Bashungwa alisema, “Hakuna soko endelevu na lenye uhakika kama soko la ndani. Kwa hiyo, wazalishaji wa ndani wazalishe bidhaa zenye ubora, na Watanzania wapende kununua bidhaa za ndani. Kwa njia hiyo, tutaimarisha soko la ndani na kulinda viwanda vyetu.”

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TanTrade, Dk. Ngw’anza Kamata alisema kutokana na changamoto ya COVID 19, mwaka huu idadi ya washiriki imepungua kiasi, “Washiriki wa ndani wamepungua kutoka 3,250 hadi 2,837 wakati wa washiriki wa nje nao wamepungua kutoka 520 hadi 43.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

Habari Mchanganyiko

Mume auwa mke kwa kumchoma visu, ajisalimisha Polisi

Spread the loveJACKSON Kalamji (49), anashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Mwanza,...

error: Content is protected !!