August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Mkuu aipiga ‘stop’ Wizara upandishaji hadhi Loliondo

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kutoanza kazi ya upandishaji hadhi mapori tengefu ikiwemo Loliondo hadi pale itakapokutana na wananchi na wadau kufanya tathimini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Majaliwa amesema ni Rais pekee ndiye anayeweza kutangaza kupandisha hadhi mapori tengefu kuwa mapori ya akiba baada ya taratibu zote za kisheria kufuatwa ikiwemo kufanya tathimini ya kina ya umuhimu wa maeneo hayo na ushirikishaji wananchi wa vijiji na maeneo yalipo.

Majaliwa ameyasema hayo leo Alhamisi tarehe 30 Juni, 2022 Bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba ya kuhitimisha Bunge.

Amesema lengo la kufanya tathimini na ushirikishwaji ni kuisadia Serikali kufanya maamuzi sahihi endapo maeneo hayo yanafaa kupandishwa hadhi au la.

“Hivyo naomba niwahakikishie wananchi wa maeneo hayo wakiwemo wa Loliondo kwamba utaratibu wa kupandisha mapori hayo kuwa mapori ya akiba utasubiri utaratibu wa mapitio ya pamoja kati ya Serikali na wananchi hivyo Wizara isianze kazi hiyo ili kupata wadau na wananchi watoe maoni yao kwa maslahi ya pande zote mbili, “amesema Majaliwa.

Amesema lengo la kupandisha hadhi mapori hayo ni kuingeza ulinzi wa rasilimali muhimu zilizopo katika mapori hayo kwa uhifadhi endelevu.

Katika hatua nyingibe Majaliwa amesema zoezi la uwekaji wa vigingi katika eneo la kilometa za mraba 1,500 la Pori Tengefu la Poloreti-Loliondo ambalo limekamilika kwa asilimia 100 halitoathiri maendeleo ya wakazi waishio kwenye eneo la vijiji 14 vinavyopakana na eneo hilo.

Hata hivyo, Majaliwa amesisitiza kwamba hakutakuwepo na kijiji chochote kitakachofutwa na hakuna miundombinu itakayoondolewa kwa kuwa ndani ya eneo la kilometa za mraba 1,500 hakuna miundombinu yoyote.

Amesema Serikali imeendelea kushirikiana na wananchi wa Loliondo katika kuboresha malisho ya mifugo, uchimbaji wa visima vya maji, ujenzi wa majosho pamoja na miundombinu ya kunyweshea mifugo kwenye eneo la kilometa za mraba 2,500.

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa

“Pia, ninaielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa Sheria ya Ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 inatumika ipasavyo kutenga na kuweka mipaka ya vijiji.”

Amesema Serikali kwa kuzingatia matakwa ya wananchi hasa maeneo ya malisho kwenye vijiji 14 vilivyopo karibu na Pori Tengefu la Poloreti itaweka utaratibu utakaopangwa kwa pamoja baada ya kukamilisha zoezi la utambuzi wa mifugo kwenye vijiji husika.

Majaliwa amesema katika kuhakikisha uwepo wa matumizi endelevu ya Pori Tengefu la Poloreti, Serikali ilielekeza eneo la kilometa za mraba 1,500 lihifadhiwe na eneo lililobaki la kilometa za mrada 2,500 wananchi waendelee kulitumia kwa shughuli nyingine.

error: Content is protected !!