October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Mchengerwa aonya mavazi yasiyo rasmi, matumizi ya simu ofisini

Spread the love

 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora nchini Tanzania, Mohamed Mchengerwa amewataka watumishi wa umma kuzingatia mwongozo wa mavazi kwa wanapokuwa mahala pa kazi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Bariadi … (endelea).

Mchengerwa amesema hayo jana Ijumaa, tarehe 8 Oktoba 2021, mkoani Simiyu alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa mkoa huo, akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Alisema, mwongozo huo wa watumishi wa umma kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Umma Na.6 wa Mwaka 2020 unatoa maelekezo ya aina gani ya mavazi yanahitajika.

Waziri huyo alisema, kuna baadhi ya watumishi wa umma katika taasisi mbalimbali za umma hawazingatii mwongozo huo na badala yake wanavaa mavazi yasiyostahili sehemu za kazi.

“Nawataka watumishi wote wa umma nchini kuzingatia mwongozo wa mavazi kwa kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Umma Na.6 wa Mwaka 2020 wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao kwani kuna baadhi ya watumishi hawauzingatii mwongozo huu na kuvaa wanavyojisikia wao, jambo hili sitaki kuliona,” alisema Mchengerwa.

Alisema, mwongozo huo unafafanua aina ya mavazi yanayoruhusiwa na yasiyoruhusiwa kuvaliwa na mtumishi wa umma kulingana na eneo alilopo wakati akitekeleza majukumu yake.

Aidha, Mchengerwa alitumia fursa hiyo kuwataka watumishi kuacha matumizi ya simu wanapowahudumia wateja kwani kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa wananchi wanaofuata huduma na kuijengea taswira mbaya Serikali kwa wananchi wake.

“Kuna baadhi ya watumishi wamekuwa wakitumia simu na hata wakiona wateja bado wanaendelea kufanya hivyo badala ya kuwahudumia, ninawataka muache tabia hiyo mara moja, tufanye kazi kwa weledi, tujitoe kwa ajili ya wananchi, tuwasilikilize wananchi wanapofuata huduma, tuwajali maana nchi hii ni yao na tupo kazini kwa ajili yao,” alisema Mchengerwa,

error: Content is protected !!