July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Mbarawa atimua wanne Mwanza

Spread the love

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, amewasimamisha kazi watumishi wanne wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSC) mkoa wa Mwanza, kupisha uchunguzi kutokana na matumizi mabaya ya mali za umma. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Watumishi waliosimamishwa kazi ni Meneja wa Kampuni hiyo, Fabian Mayenga, Afisa Manunuzi, Abdallah Rumila, Mwanasheria wa Kampuni, Josephat Mushumbusi na Meneja Miradi wa Kampuni hiyo, Alex Mchaum.

Watumishi hao wanatuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali za kuingizia Serikali hasara ya mamilioni ya shilingi katika kampuni hiyo ya meli ambayo imeonekana kupoteza mwelekeo kwa hivi sasa.

Meneja wa kampuni hiyo, Fabian Mayenga, amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kushindwa kusimamia fedha kiasi cha Sh. 600 milioni zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya matengenezo ya Meli ya MV Victoria ambayo kwa sasa haifanyi kazi.

Kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na Serikali kwa ajili ya matengenezo ya meli hiyo, walikitumia katika kujilipa mishahara ya wafanyakazi bila kibali maalumu kutoka serikalini kitendo ambacho kimesababisha kusimama kwa matengenezo ya meli hiyo.

Waziri Mbarawa, alitaja tuhuma nyingine wanazokabiliwa nazo kuwa ni pamoja malipo makubwa ya bima ya meli ya MV Victoria, ambayo haifanyi kazi pamoja na kushindwa kufanya matengenezo ya injini ‘blocks’ ya meli ya MV Butiama.

Mbarawa amesema kuwa majibu wanayotoa watumishi hao hayaendani na ukumbwa wa tuhuma zinazowakabili, kwani licha ya Serikali kuwaamini na kuwapa nafasi lakini bado walishindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa.

Amesema kuwa watumishi hao wa umma wameshindwa kuwa waaminifu na mali za Wananchi kitendo ambacho kimesababisha meli za kampuni hiyo kusimama hususani MV Victoria kushindwa kufanya kazi kama kawaida licha ya kutolewa kwa fedha za matengenezo ya awali.

“Vijana kama hawa ndiyo wanaamua kufanya mambo makubwa kama haya, watu hawa wanapaswa kusimamishwa kazi na kupisha uchunguzi ufanyike wa haraka na kama watakutwa na makosa hatua zichukuliwe juu yao.

“Ninaomba taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wafanye uchunguzi mara moja kuhusiana na suala hili, hawawezi kujiamulia kutumia fedha bila kupewa kibali kutoka mamlaka husika na kutukaendeleakuwa nao,” amesema Mbarawa.

Hata hivyo amesema kuwa mamlaka ya meli inapaswa kutoa matangazo ya kazi ili watu wengine wenye uwezo wa kufanya kazi waweze kufanya na kuachana na wale wasiokuwa waaminifu na mali za umma kwani kuendelea nao kutasababishataifa kurudi nyuma kimaendeleo.

Pia amesema matumizi mabaya ya fedha za umma unaofanywa na watumishi wasiokuwa waaminifu imekuwa ni tatizo katika ukuaji wa maendeleo ya Taifa, hivyo taasisi za Serikali zinapaswa kuacha kufumbia macho watu wa namna hiyo.

Naye Meneja wa Kampuni hiyo akizungumza kwa niaba ya watuishi hao, Fabian Mayenga, amesema kuwa juhudi za kutengeneza injini Blocks ya Meli ya MV Butiama, zilishafanyika lakini baada ya wataalamu kundua tatizo ni kubwa waliamua kuacha nayo.

“Lengo la Engine Blocks ya Mv Butiama ilikuwa ni kuichonga na kurudi katika taratibu za kawaida, kwa bahati mbaya uchangaji ule haukufuata utaratibu mzuri hivyo sualalake likashindikana,” amesema Mayenga.

Mayenga amesema kuwa hadi sasa haifahamiki kama injini ya MV Butiama inaweza kufanya kazi kwani juhudi za kuifanyia matengenezo zilizofanyika ni kubwa nakwamba walijilizisha na kufahamu haitaweza kurudi kuendelea kufanya kazi.

error: Content is protected !!