November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Makamba ahudhuria warsha ya mradi wa  kusindika gesi asilia Norway

Spread the love

WAZIRI wa Nishati, January Makamba, ameshiriki katika warsha ya viongozi iliyofanyika kwenye mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia (Liquefied Natural Gas Plant – LNG) wa Equinor. Mradi huo  upo Kaskazini mwa Norway kwenye mji wa  Hammerfest. Anaripoti Mwandishi Wetu, Norway … (endelea).

Warsha hiyo iliwashirikisha  pia Balozi wa Tanzania kwenye nchi za Nordic, Grace Olotu; Balozi wa Norway nchini Tanzania  Elisabeth Jacobsen; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali.

Aidha uongozi wa juu wa kampuni ya Equinor, imetoa nafasi kwa viongozi hao kujadili maandalizi ya mradi  wa kuchakata na kusindika gesi asilia Tanzania wenye thamani ya shilingi trilioni  70 utakaofanyika  mkoani Lindi.

Viongozi hao wametumia  fursa hiyo kukutana  na wafanyabiashara wa eneo hilo wanaonufaika kwa kutoa huduma kwenye eneo hilo la mradi wa Equinor, Hammerfest. Pia kukutana na Watanzania wanaofanya kazi katika mradi huo.

Mtambo uliojengwa kwenye mradi huo wa Equinor  huchakata bilioni 4.6 za mita za ujazo za gesi asilia kwa mwaka ikiwa ni pamoja na bidhaa nyingine kama gesi ya kupikia (LPG).

Waziri Makamba amewahakikishia Equinor na washirika wake kuwa Serikali ya Tanzania, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha kuwa majadiliano yote ya msingi kuhusu mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia nchini yanakamilika ifikapo Desemba mwaka huu.

error: Content is protected !!