January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Mahenge azomewa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binirth Mahenge

Spread the love

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binirth Mahenge, amejikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wabunge kutokana na kuunga mkono uongozi wa mkoa wa Kigoma kutoza ushuru mkubwa katika biashara ya mkaa. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Hali hiyo ilijitokeza bungeni baada ya mbunge wa Mhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) kuuliza swali la nyongeza akitaka kujua ni kwanini uongozi wa mkoa huo wamepandisha ushuru kutoka Sh. 3,000 hadi Sh. 25,000.

Akijibu swali hilo, Dk. Mahenge, amesema kuwa ni jambo pekee la kusifiwa kwa viongozi wa Kigoma kupandisha ushuru kwani kwa kufanya hivyo wataweza kukomesha ukataji wa kuni na uchomaji wa mkaa.

Kauli hiyo ya Dk.Mahenge, ilisababisha wabunge wengi bila kujali itikadi za vyama kumzomea huku Spika wa Bunge, Anne Makinda akimkingia kifua na kumtaka aendelee kujibu.

Wabunge hao waliendelea kumzomea lakini yeye alisema kuwa njia pekee ya kuweza kukabilana  na uharibifu wa mazingira ni pamoja na kuweka ushuru mkubwa.

Mbali na hilo, amesema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa wananchi kutumia majiko banifu ambayo yanatumia mkaa kidogo.

Aliendelea kuhamasisha wananchi watumie umeme wa gesi ambao amesema kuwa mpaka sasa ni umeme ambao unapatikana kwa bei nafuu.

Awali katika swali la msingi la mbunge wa viti maalum, Makilagi Nassoro (CCM), alihoji serikali ina mkakati gani wa wanawake katika masuala ya upandaji wa miti na kwamba serikali imejipangaje kuhakikisha inawawezesha wanawake ambao wanatumia kuni jambo ambalo limekuwa likisababisha uharibifu wa mazingira.

Katika kujibu swali hilo, Naibu wazari, Stevin Masele alisema kuwa serikali imekuwa ikishirikiana na wanawake na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanapatiwa elimu juu ya upandaji wa miti.

error: Content is protected !!