October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Madini: STAMICO imeingia kundi la wawekezaji

Spread the love

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko amesema Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeingia kwenye kundi la wawekezaji baada ya kufanikiwa kukuza mtaji wake wa uwekezaji na kufikia Sh bilioni 63.9 jambo ambalo katika miaka iliyopita halikuwepo. Anaripoti Julianna Assenga -SJMC … (endelea).

Amesema Shirika hilo ambalo sasa linasherehekea kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1972, ni dhahiri linawekeza kwa niaba ya nchi.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Venance Mwase akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema hatua hiyo imetokana na ubunifu uliofanywa na Menejimenti ya Shirika hilo huku Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiongezea nguvu kuhakikisha shirika hilo ambalo lilikuwa katika orodha ya mashirika ya umma yanayotakiwa kufutwa, sasa linafufuka.

Biteko ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam leo tarehe 10 Agosti, 2022 baada ya kutembelea kiwanda cha majaribio  kinachotengeneza Mkaa Mbadala (Rafiki Briquettes) ambao ni mahsusi kwa ajili ya kulinda mazingira.

STAMICO wameshirikiana na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) katika kubuni mkaa huo ambao ni muarobaini wa matumizi ya kuni au mkaa unaotokana na miti kupikia.

“Mkaa huu unaweza kuivisha chakula haraka kuliko mkaa wa miti, lengo letu ni kufunga mitambo ya kuzalisha mkaa mbadala kila mkoa… hivyo tutaanza kufunga Kibaha na Songwe, nia yetu ni kuwafanya watanzania walinde mazingira,” amesema.

Aidha, amelipongeza Shirika hilo kwa kupiga hatua hasa ikizingatiwa mwaka 2018 almanusura lifutwe kwa kuwa lilikuwa likiingizia hasara serikali.

“Lakini Menejimenti imefanya kazi nzuri na hata uwekezaji wake umepanda… limewekeza bilioni 63.9, huko nyuma haukuwepo lakini sasa imetengeneza faida.

“Nawapongeze sana bodi na mtendaji mkuu (Dk. Venance Mwase) na timu yake kwa kuja na mawazo mapya na kuacha kulalamika. Shida iliyopo mashirika ya umma hatufanyi shughuli zetu kibiashara.

“STAMICO wamefufua hata mgodi wa Kiwira unaozalisha makaa ya mawe. Mgodi huu ulisimama tangu 2008, sasa umefufuka na wanachimba zaidi ya tani 30,000. Kulikuwa na nyumba 300 ambazo zilitelekezwa na kuwa maghofu lakini STAMICO wamekarabati nyumba zaidi ya 100 ambazo watu wanaishi.

“Watu wa Kiwira wanapatiwa maji umeme, madaraja yamejengwa na mengine kukarabatiwa.. maboresho haya yote ni kwa sababu ya uwepo wa STAMICO ni dhahiri shirika hili limeingia kwenye kundi la wawekezaji na kweli wanawekeza kwa niaba ya nchi,” amesema

Amesema hivi karibuni STAMICO wanatarajia kununua mitambo ya kutengeneza mkaa mbadala pamoja na mingine 11 ya uchorongaji na mitambo minne ya kuchimba madini.

“Ni uwekezaji ambao STAMICO wamefanya, nawapongeza kwa ubunifu wao. Natamani tunaposherehekea miaka 51 ya shirika mwaka ujao tuwe na vitu vingi zaidi vya kuwaonesha,” amesema.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dk. Venance Mwase amesema katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya shirika hilo yanayotarajiwa kufanyika jijini Dodoma tarehe 12 Agosti, 2022, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.

Amesema katika maadhimisho hayo wanatarajia kupanda miti 10,000 nchi nzima kwa kuanza na mkoa wa Dodoma.

Akizungumzia ubunifu wa mkaa huo amesema mitambo iliyoagizwa kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa huo katika mikoa ya Pwani na Songwe ina uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa.

“Katika bajeti ya mwaka huu tumeagiza pia mitambo ya kuzalisha mkaa mbadala ambayo itafungwa Dodoma na Mwanza, lakini kila mkoa utafungwa mitambo ya kuzalisha mkaa huo kwa maana hiyo kila mkoa kutakuwa na viwanda vya kuzalisha mkaa mbadala.

“Ni juhudi za shirika katika kuunga mkono mikakati ya Serikali kuwa nchi ya viwanda. Mafanikio mengine ndio kupata nishati mbadala inayotunza mazingira,” amesema.

error: Content is protected !!