April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Kigwangalla aeleza corona ilivyoivuruga sekta ya utalii

Watalii wakiwa moja ya mbuga nchini Tanzania

Spread the love

WAZIRI wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Dk. Hamisi Kigwangalla amesema madhara ya kuwepo kwa ugonjwa wa corona yanaonekana kuwa makubwa zaidi na kuna dalili za kushuka kwa mapato yaliyotarajiwa kukusanywa na taasisi kubwa zilizo chini ya wizara hiyo. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Kigwangalla ameyasema hayo leo tarehe 7 Mei 2020 bungeni Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya wizara ya maliasili na utalii kwa mwaka wa fedha 2019/20 pamoja na kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2020/21.

Amesema kabla ya madhara hayo sekta ya utalii ilikuwa ikichangia asilimia 25 katika mapato yote ya kigeni inayopata nchini na imeathiriwa zaidi kutokana na ukweli kwamba inategemea zaidi mapato ya watalii wanaotoka nje ya nchi ambao kwa sasa kutokana na ugonjwa huo, wameshindwa kusafiri na wengi wao wamesitisha safari za kuja nchini kutalii. 

Aidha, ameeleza ili kuona madhara ya awali ya ugonjwa huu, wizara ilifanya tathmini ya awali iliyojikita katika kipindi cha tangu ugonjwa huo uanze hadi tarehe 06 Aprili, 2020. Tathmini hiyo ilibaini kuwa;

Madhara makubwa ya corona katika sekta ya utalii yalianza kuonekana mwanzoni mwa Machi, 2020 tofauti na miezi ya Februari na Januari, 2020 ambapo hali ilikuwa shwari na tathmini imebaini mashirika 13 ya ndege yalisitisha kuja nchini tangu tarehe 25 Machi, 2020 na hivyo kuondoa uwezekano wa kuendelea kupata watalii kutoka nje ya nchi.

Mashirika yaliyositisha safari zake ni pamoja ni: Emirates, Swiss, Oman air, Turkish, Egyptian air, South African Airways, Rwandair, Qatar, Kenya Airways, Uganda Airlines, Fly Dubai na KLM. Vilevile, kampuni yetu ya ndege ya Air Tanzania imesitisha safari za nje ya nchi.

“Madhara haya yanaonekana kuwa makubwa zaidi ambapo tayari kuna dalili za kushuka kwa mapato yaliyotarajiwa kukusanywa na taasisi kubwa zilizo chini ya wizara ambazo ni TANAPA, NCAA, TFS na TAWA.”

WAZIRI wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Dk. Hamisi Kigwangalla

“Kwa mfano, katika mwaka 2020/2021 TANAPA ililenga kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 363.9, lakini kutokana na hali inavyoendelea makisio sasa yanakadiriwa kuwa Shilingi bilioni 64 au chini ya hapo; NCAA ilikadiria Shilingi bilioni 162.7, sasa ni Shilingi bilioni 58; TFS ilikadiria Shilingi bilioni 153.6, sasa ni Shilingi bilioni 121; na TAWA ilikadiria Shilingi bilioni 58.1, sasa ni Shilingi bilioni 22,” amesema.

Amesema hata kama hali itatulia mwezi Oktoba, 2020, idadi ya ajira za moja kwa moja katika sekta ya utalii zitashuka kutoka 623,000 zilizotarajiwa hadi kufikia 146,000; watalii watashuka kutoka 1,867,000 waliotarajiwa hadi kufikia watalii 437,000.

“Mapato yanayotokana na utalii yatashuka kutoka Shilingi trilioni 2.6 zilizotarajiwa hadi kufikia Shilingi bilioni 598. Upungufu huo wa mapato ni mkubwa kwa sekta na unaweza kusababisha baadhi ya taasisi za uhifadhi zilizo chini ya wizara kushindwa kujiendesha ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara.

“Katika kukabiliana na hali hiyo, wizara imeendelea kuwashirikisha wadau wa sekta ili kuweka mikakati ya namna ya kuisaidia sekta isiathirike zaidi,” amesema.

error: Content is protected !!