November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Kabudi ‘ashikwa kooni’ kutema uwaziri

Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Spread the love

PROFESA Paramagamba Kabudi, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, ametakiwa kujiuzulu kwa madai ya kushindwa kumshauri vizuri Rais John Magufuli. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 15 Mei, 2019 na Anthony Komu, Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), wakati akichangia Hotuba ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2019/20.

Mbunge huyo amesema, Prof. Kabudi alishindwa kutekeleza wajibu wake wa kumshauru rais na hivyo kulisababishia taifa hasara, kutokana na kuingia makubaliano ya Kampuni ya Kenya ya Window Power kwamba, ilikuwa yenye ueledi na uwezo.

Kampuni hiyo, ilitetewa na Prof. Kabudi na kuingia nayo mkataba wa kununua korosho ambapo baada ya miezi mine, imeshindwa kutekeleza huku ikitajwa kuwa ya kitapeli.

Januari 2019 Kampuni hiyo ya Kenya alijinadi kununua tani 100,000 za korosho zenye thamani ya shilingi 418 bilioni, hata hivyo tarehe 9 Mei 2019 serikali imeeleza kuwa, kampuni hiyo imeshindwa kutekeleza makubaliano ya kimkataba.

Hata hivyo Kom amesema kuwa, ili kulinda viwanda ni lazima kuwa na mazingira yanayotabirika na kwamba, Tanzania kuna tatizo la mazingira ya biashara.

“Mwezi huu tu uliopita, Mheshimiwa Naibu Spika, TRA walitoa tangazo la kupiga marufuku vinywaji vyote ambavyo havina stika ya elekitroniki kuwa ifikapo 30 ya mwezi uliopita, vinywaji vyote vitakuwa vimekoma na havitakuwa na thamani tena.

“Sasa Mheshimiwa Naibu Spika, wale waliopiga marufuku sijui walizingatia nini kwasababu, hivyo vinywaji vilinunuliwa kwa kufuata utaratibu wa kisheria na vina stika ambazo zinatambulika na vimeishasambazwa nchi nzima,” amesema Kom na kuongeza;

“Maana yake vinywaji hivi vinapatikana Dar es Salaam na tuseme vinapelekwa kwenye jimbo fulani labda kwa ndugu yangu Mlimba, kule Ifakara na unapowaambia wavirejeshe kwa siku 30, unakuwa unafanya jambo la ajabu.”

Amesema kuwa, mazingira ya kufanya biashara ni magumu zaidi kutokana na kuwepo kwa mlolongo wa kuwepo kwa mlolongo mkubwa wa tozo.

https://www.youtube.com/watch?v=WRj2IrKh9j0

Hussein Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM) amesema, kuna ukiritimba mkubwa katika utoaji wa vibali kwa wawekezaji wanaoanzisha viwanda nchini.

Na kwamba, ili kuondokana na adha hiyo iliyopo katika mlolongo wa utoaji vibali kutoka taasisi mbalimbali za serikali, ameshauri serikali kuweka mfumo wa pamoja kwa taasisi hizo zinazokusanya tozo na kutoa vibali.

“Kama tutajenga reli, barabara tutaleta umeme vyote hivi vikakosa biashara ya kuvifanya viwe effective (viendelee kufanya kazi), havitakuwa na maana…Kampuni inayotaka kufanya biashara ya maua na bidhaa zingine, anahitaji jumla ya vibali 45,” amesema Bashe.

Bashe ameishauri serikali kutumia taarifa ya Shirika la Fedha la Duniani (IMF), ambayo ilitoka awali kwa sababu ina ushauri mzuri.

Amesema, taarifa hiyo inatoa ushauri kwamba kama Tanzania inataka kukuza uchumi kwa asilimia saba, kuna mambo manne ya kufanya na kuwa, taasisi zinazohusika na biashara kama Brela, TFDA, NEMC, TBS na zingine kuwa katika eneo moja kurahisisha vibali kutolewa.

Julius Karanga, Mbunge wa Monduli (CCM) amesema, hakuna ushirikiano kwenye wizara za serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Hivi kuna mwekezaji gani anayeweza kwenda kuchukua magadi wakati hakuna hata kilometa moja ya barabara iliyojengwa kuelekea kwenye mradi? Ni bora muwaambie wananchi wetu waendelee kuyatumia maeneo yao ambayo wameyatoa kwa bei rahisi,” amesema.

Ahmed Shabiby, Mbunge wa Gairo amesema, “kuna kukomoana kwenye biashara, watu wanapigwa faini zisizostahili, waziri wa viwanda upo, sasa wewe kazi yako ni nini? Kila mtu siku hizi amekuwa ni mkusanya kodi.

“Mimi nataka nijue, maana ya kuwa waziri ni kukuza biashara, si kuua biashara, nikushauri mheshimiwa waziri ingilia popote ambapo mfanyabaishara anaonewa,” amesema Shabiby.

error: Content is protected !!