HAWAKUTARAJIA. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Seleman Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI), kuyumba katika kauli zake kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).
Waziri Jafo amekuwa akitoa kauli zinazoashiria kiwewe, kutokana na vyama vya upinzani kugomea uchaguzi huo, kwa madai ya kuchafuliwa na wasimamizi.
Tayari ametoa kauli zaidi ya tatu kuhusu jambo moja – uchaguzi huo – na zote zimepishana. Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019.
Tarehe 7 Novemba 2019
Muda mfupi baada ya Chadema kutangaza kujitoa Waziri Jafo alisema, uamuzi huo (wa Chadema) unawanyima fursa wagombea wa chama hicho waliopitishwa, waliokata rufaa kupinga kuenguliwa.
Akaonesha kusikitishwa kwamba, ni haki yao (Chadema) kujitoa huku akisisitiza kuwa kanuni za uchaguzi huo, hazijafunga mtu yeyote kukata rufaa.
Tarehe 9 Novemba 2019
Baada ya msimamo huo kutikisa na vyama vyingine kupita mlango huo, Waziri Jafo akaja na kauli nyingine kwamba vyama vya siasa ndivyo vilivyojitoa na si wagombea.
Akimaanisha kwamba, wagombea wataendelea na mchakato hata kama vyama vimejiondoa. Hapa alijitenga na Katiba ya Jamhuri inayoelekeza kuwa, kila mgombea lazima atokane na chama cha kisiasa.
Tarehe 10 Novemba 2019
Waziri Jafo mbele ya waandishi wa habari jijini Dodoma, alitangaza kuwarudisha wagombea wote wa serikali za mitaa ambao walichukua fomu na kuzirejesha. Hapa hakutaka kuangalia udhaifu wowote uliojitokeza kwenye fomu hizo, kigezo kilikuwa kurejesha fomu tu.
Ule upungufu ulioanishwa na wasimamizi wa uchaguzi huo, uliosababisha zaidi ya asilimia 80 ya wagombea wa wapinzani kung’olewa, kwa kauli hiyo Waziri Jafo aliupuuza.
Tarehe 11 Novemba 2019
Waziri Jafo ‘akachenji gia tena,’ safari hii alizika kauli yake ya awali kwamba kila aliyechukua fomu na kurudisha, basi aingizwe kwenye mchakato na badala yake sasa, ameelekeza watakaoingia kwenye mchakato ni wale walioteuliwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi pekee.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ndio chama cha kwanza kutangaza kususia uchaguzi huo kwa madai ya dhuluma inayosimamiwa na wasimamizi wa uchaguzi huo.
“Jiji la Dar es Salam leo tumebakiziwa mitaa 24, upumbavu gani huu.., tukashiriki mitaa 24 kati ya mitaa 570 ya jiji la Dar es Salaam? Hali ndiyo hiyo hiyo kwenye jiji la Mwanza, Mbeya, Arusha na kwenye mikoa yote,” alisema Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho wakati akitangaza uamuzi wa kujitenga kwenye uchaguzi huo.
Chama cha ACT-Wazalendo kilifuata uamuzi wa kujitenga, kisha vikafuata Chama cha NCCR-Mageuzi, Chaumma, UPDP ambapo CUF imeeleza kutafakari hatua hiyo.
Katika mazingira ya namna hii, bila shaka uchaguzi unaweza kufanywa wa upande mmoja, na huo hauwezi kuitwa uchaguzi bali uchafuzi.
Leave a comment