October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Gwajima kumuwakilisha Rais Samia kongamano la wanawake Urusi

Dk. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Spread the love

 

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima anatarajia kumuwakilisha Rais wa Samia Suluhu Hassan katika Kongamano la tatu la Kimataifa la Wanawake litakalofanyika nchini Urusi kwa siku tatu kuanzia Oktoba 13-15, 2021. Anaripoti Danson Kaijage (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 12 Oktoba 2021 na wizara hiyo ya afya, Dk.Gwajima akiwa nchini Urusi, atashiriki katika ufunguzi wa kongamano hilo na kuelezea namna Tanzania imefanikiwa katika masuala ya usawa wa kijinsia.

Pia ataelezea namna ilivyowainua wanawake kiuchumi na kutambua mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

Dk. Gwajima atashiriki katika kongamano hilo ikiwa ni mwelekeo wa  Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha uwepo wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika nyanja mbalimbali unaendelea kuimarika.

Aidha, lengo kuu la kongamano hilo ni kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya dunia na kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia.

Vile vile, Dk. Gwajima atakutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Afya wa Urusi kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano katika Sekta ya Afya yakiwemo mapambano dhidi ya virusi vya UVIKO19 duniani.

“Kongamano hili litaambatana na mikutano mbalimbali inayolenga masuala kadhaa yakiwemo mapambano dhidi ya virusi vya UVIKO19, uwezeshaji wanawake kiuchumi na kuwezesha usawa wa kijinsia.

“Kongamano la kimataifa la wanawake nchini Urusi litajumuisha viongozi kutoka mataifa mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali, wabunge, mashirika ya kimataifa, wakuu wa mitandao ya kimataifa ya wanawake na wawakilishi wa makampuni  ya kibiashara duniani” taarifa imeeleza.

error: Content is protected !!